
AKIENDELEA kukisuka kikosi chake, Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa, bado mipango yake ipo vilevile ya kulichukua Kombe la FA na kumaliza Ligi Kuu Bara wakiwa katika nafasi ya pili.
Yanga, juzi ilianza mazoezi ya pamoja ya timu hiyo tayari kujiandaa na ligi iliyorejeshwa baada ya kusimama kwa zaidi ya mwezi mmoja tangu serikali itangaze kusimamisha ili kupisha maambukizi ya Virusi vya Corona.
Timu hiyo imeanza mazoezi yake bila ya Kocha Mkuu, Luc Eymael aliyepo nchini kwao akisubiria ndege kuruhusiwa kuanza kufanya kazi baada ya baadhi kufunga mipaka kutokana na Corona Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkwasa alisema kuwa bosi wake, Eymael tayari amemtumia program za mazoezi zenye malengo ya kuiandaa timu itakayofanya vizuri katika ligi na FA katika kipindi ambacho yeye hayupo nchini.

Mkwasa alisema tayari ameanza program hizo za mazoezi na aliyoanza nayo ni ya fi tinesi kwa ajili ya kuuandaa mwili kabla ya kuhamia yale ya kiufundi jinsi ya kulinda goli lao na kushambulia.
Aliongeza kuwa lengo la kuchukua nafasi ya pili katika ligi na kulibeba Kombe la FA ni kushiriki michuano ya kimataifa, mwaka huu na hilo linawezekana kwao kutokana na ubora wa kikosi chao Kauli hiyo inaendana na jinsi ambavyo wameanza mazoezi hayo kuanzia juzi, ambapo wachezaji na benchi la ufundi wote wanaonekana kuwa makini na kile wanachokifanya huku muda mwingi wakiwa hawana utani wakati wa mazoezi.
“Nimewasiliana na kocha na kuzungumza mambo mengi, kati ya hayo ni mikakati waliyoiweka awali kabla ya ligi kusimama kupisha Corona ambayo ilikuwa ni kumaliza ligi katika nafasi ya pili na kuchukua Kombe la FA
“Kwani malengo yetu ni kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa, licha ya kuwepo timu Tanzania katika mashindano hayo ya kimataifa kutokana na baadhi ya nchi ligi zao kusitishwa kutokana na Corona.
“Lakini hilo hatutaliangalia na badala yake tutahakikisha tunapambana ili tutimize malengo yetu hayo tuliyojiwekea na hilo linawezekana kwetu kwani wachezaji wenyewe wametuhakikishia kupambana,” alisema Mkwasa.
Stori: Wilbert MolandiDar es Salaam