×

VIDEO: Shigongo Afundisha Somo Muhimu Kuhusu Tabia

MHAMASISHAJI maarufu Afrika Mashariki na Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Global Group, Eric Shogongo, amefundisha somo muhimu la jinsi ya kuibadili tabia ili uweze kufanikiwa maishani.

Akizungumza leo kwenye Kipindi cha Darasa kinachorushwa kila siku kupitia +255GlobalRadio, Shigongo alisema, ili uweze kufanikiwa maishani lazima uchague kuziacha tabia fulani mbaya ambazo ndizo zinawakwamisha wengi.
“Tunapozaliwa hapa duniani huwa hatuji na tabia, tunazikuta hapa hapa duniani.

Mtu anapokuwa na tabia fulani lazima tujiulize hii ameitoa wapi? Zipo tabia ambazo tumezijenga sisi wenyewe. Unakuta mtoto anafanywa kama yai kwa sababu nyumbani kuna kila kitu, huyo mtoto atakuwa na tabia ya uvivu,” alisema Shigongo.

Alisema, unachotakiwa kufanya ni kukaa chini peke yako na kuanza kung’amua nini kinachokusumbua kwenye maisha yako kisha ukifanyie kazi.

“Ukiwa bafuni unajua kabisa nini kinakukwamishaga. Mimi bwana nikiacha matumizi mabaya nimejenga, mimi nikiacha uvivu nimejenga. Mtu akinitazama hata mimi kuna tabia fulani inanisumbua. Hakuna kitu kinanitesa kwenye maisha yangu kama kukiacha kitanda changu lakini tabia hiyo naifanyia kazi mpaka sasa,” alisema Shigongo.


Alisema, kinachowafanya watu washindwe kufanikiwa maishani ni kutokana na jinsi walivyoamua kuchagua kufanya mambo mabaya.

“Haupo hapo ulipo kwa bahati mbaya, upo hapo kwa sababu ya mambo fulani ambayo umekuwa ukiyafanya, ukiyaacha hayo utafanikiwa. Masanja (Emmanuel Mgaya, mchekeshaji) alizaliwa huko kijijini Ubaruku sijui kijiji gani huko…amepambana hadi leo anatumia magari ambayo wanayatumia matajiri,” alisema Shigongo.

Alisisitiza jinsi ya kuachana na tabia fulani mbaya ni kuiacha taratibu kama vile ambavyo mtu fulani aliianza.
“Jinsi ya kuiua tabia uliyoitengeneza kwa muda mrefu ni kazi moja ngumu sana. Tabia huwa unaiua taratibu kama vile ulivyoianza taratibu.

“Mtu alikuwa anavuta sigara 20, ananunua pakti moja anavuta 18 anatupa mbili…anaendelea kupunguza kidogo kidogo mpaka siku moja akazitupa zote,” alisema na kuongeza:
“Siri kubwa kabisa ya mafanikio ni good character, utengeneze tabia njema. Ni kazi sana kuwa na tabia njema lakini ni lazima uifanye, ukiifanya kwa siku 40 mfululizo inakuwa ni sehemu ya maisha yako,” alisema.
Unaweza kumfuatilia Shigongo kwenye kipindi hicho Jumatatu kuanzia saa 10 kamili jioni. Zaidi fuatilia mitandao ya kijamii Instagram, Facebook na Twitter @255GlobalRadio au kupitia tovuti ya www.globalradio.co.tz

Leave a Comment