×

Asha Baraka: Nipo tayari kuajiriwa na Mwinjuma Muumini

AMA kweli aliye juu msubiri chini, ndivyo unavyoweza kuitafsiri kauli ya Mmiliki wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ Asha Baraka ambaye amesema yupo tayari kuajiriwa na Mkurugenzi wa Bendi ya Shadai, Muumin Mwinjuma.  Muumin Mwinjuma pamoja na wasanii wengine wakali kama vile Ally Choki, kwa miaka kadhaa walikuwa wameajiriwa na Asha Baraka kwa kupitia bendi zake za Twanga na African Revolution ‘Tamtam’.

Maamuzi ya Asha kukubali kuajiriwa na Muumini, yamekuja siku chache baada ya Asha kumuomba staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ kuwasaidia wanamuziki wa dansi nchini ili waufufue muziki huo. Hata hivyo, maombi hayo ya Asha kwa Mondi, yaligeuka shubiri kwake baada ya wanamuziki Muumin na Choki kumshambulia kwa nyakati tofauti katika kile walichoeleza kuwa mwanamama huyo alitakiwa kuomba msaada binafsi na si kuwajumuisha kwenye msaada huo.

Akizungumza na RISASI, Muumini alihoji; “Nani kamwambia wanamuziki wa dansi tumeishiwa kiasi cha kumuomba msaada huyo Diamond? “Asitake kutudhalilisha, wengine hatuna njaa hizo. Mimi nahisi huyo mama yetu kwa sasa yeye ndiye ameishiwa na anahitaji msaada kupitia sisi wanamuziki wa dansi,” alisema Muumini.

Katika kuonesha yuko vizuri, Muumini alimtangazia Asha, dau kwenye bendi yake ili ampe kitengo fulani cha kusimamia kutokana na uzoefu mkubwa na masuala ya kusimamia bendi na kumuahidi mkataba wa Sh milioni sita kwa miezi sita na suala la mshahara watakubaliana. “Mimi niko serious narudia tena kusema, namtaka Asha Baraka aje kwenye bendi yangu ya Shadai, nitamuajiri kwa mkataba wa Sh milioni sita kwa miezi sita na mshahara tutakubaliana ili niweze kumsaidia” alisema Muumini.

Mwanamuziki mwingine aliyeonesha kukerwa na kitendo cha Asha kuwaombea msaada huo ni Choki ambaye sasa hivi anafanya muziki kama msanii wa kujitegemea ‘solo artist’. Choki alisema kuwa, Asha kama anahitaji msaada, angetakiwa kuomba yeye binafsi na bendi yake badala ya kujumuisha wanamuziki wote wa dansi.

“Yeye kama amefulia na bendi yake, angejiombea msaada mwenyewe na siyo kutuhusisha sisi wengine. Mimi sijafikia kumuomba msaada Diamond. “Kama anamuona huyo Diamond ana uwezo mkubwa, si angeenda kumuomba ajira kwa kuwa yule jamaa sasa hivi ana vitengo vingi, anaweza akampachika popote ili ajikwamue kimaisha,” alisema Choki.

Hata hivyo, akijibu mapigo mbele ya RISASI, Asha alisema Choki na Muumini kinachowasumbua ni wivu tu, lakini ukweli ni kwamba, Diamond yuko juu na hawamfikii. Alisema wasanii hao wameshafulia, hata hivyo msaada huo wasingepewa kwa lazima kama wanavyodhani.

“Kama wao hawataki msaada, si wawaachie wenzao wengine wasaidiwe, kwani wanamuziki wa dansi wako peke yao? “Na huyo Muumini anayetaka kuniajiri kwa hilo dau la milioni sita, mwambie mimi niko tayari hata leo”.

“Akiwa tayari na hiyo pesa, aandae vyombo vya habari na aniite mimi nitakuja kusaini huo mkataba kwani mimi kuajiriwa kuna ubaya gani? “Waache wivu, muda wao umeshapita, wamuache Mondi atambe.”

STORI : Richard Bukos, Risasi

Leave a Comment