
DAR: Ni mtihani mzito! Ndivyo unavyoweza kutafsiri vihunzi watakavyokumbana navyo wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Hatua hiyo inakuja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuanika vigingi viwili kwa wagombea hao ambavyo ni rasimu ya maadili na rasimu za kanuni za uchaguzi mkuu mwaka 2020.
Vivyo hivyo kwa upande wa chama tawala – CCM, nacho kimeweka utaratibu mpya wa kupata wagombea ubunge na udiwani ambao umetafsiriwa kuwabana vilivyo wagombea watakaojitokeza katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Wakati hayo yakijiri, Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru), imeanza kukunjua makucha mapema na kunasa makada saba wa CCM, huku chama hicho kikianika namba mbili za kusaidia kupata ushahidi wa watuhumiwa wa rushwa, jambo ambalo pia limeonesha wazi kuwa mtihani mzito kwa makada wa CCM.
NEC NA RASIMU
Mei 27 mwaka huu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilikutana na viongozi wa vyama vya siasa na kujadili rasimu ya maadili ya uchaguzi kwa muda wa saa chache kisha kusaini rasimu hiyo.
Vivyo hivyo, rasimu ya kanuni za uchaguzi nayo Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage alifafanua kuwa ipo mbioni kukamilisha marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi za Madiwani, Wabunge na Urais.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo, Ado Shaibu alisema licha ya maboresho machache kufanyika ndani ya rasimu hiyo ya maadili ya uchaguzi, NEC ilivilazimisha vyama kusaini siku hiyohiyo bila kuwasilisha kwanza toleo la mwisho la maadili ya uchaguzi lililojumuisha marekebisho husika.
“Jawabu la NEC kuwa chama ambacho hakitasaini maadili ya uchaguzi siku hiyo, hakitashiriki kampeni,” alisema.
Hoja hiyo iliungwa mkono pia na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika ambaye alisema vyama vimelazimishwa kusaini maadili hayo sawa na kuwekewa shoka shingoni.
Alisema hata kama patatokea uhitaji wa kufanyika mabadiliko, hakuna kipengele kinachoruhusu vyama kusaini rasimu hiyo baada ya marekebisho.
Aidha, kihunzi kingine ambacho kimeonekana kuwa mtihani mzito kwa wagombea mwaka huu ni kanuni za uchaguzi.
Licha ya NEC kupitia mchakato wa kukusanya maoni kwa ajili ya marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi (Madiwani, Wabunge na Urais), inaelezwa kuwa NEC ipo mbioni kukamilisha kanuni hizo bila kuwepo kwa kikao cha wadau kujadili rasimu ya mwisho ya kanuni husika.
Ado Shaibu anafafanua kuwa licha ya kuwaandikia NEC maoni yao, katika nakala ya rasimu waliyopatiwa, inaonesha kuwa mawakala wanaweza kunyimwa hati za viapo kwa sababu hakuna kifungu cha kanuni kinachowalazimisha wasimamizi kutoa nakala hizo.
“Rasimu ya kanuni zote mbili, (kanuni ya 56(2) ya kanuni za Uchaguzi wa Madiwani na kifungu cha 63(2) cha Kanuni za Uchaguzi wa Wabunge na Rais), hazina sharti kwa wasimamizi wa uchaguzi kuwapa hati za viapo mawakala wa vyama vya siasa.
“Pia rasimu za kanuni za uchaguzi, zinatumia lugha ya hiyari kwa NEC kuwaalika waangalizi wa kimataifa. Kanuni hizo pia zinakataza waangalizi wa kimataifa na wa ndani kuripoti kwa vyombo vya habari mapungufu ya uchaguzi watakayoyaona wakati uchaguzi ukiendelea (Kifungu cha 20 (2)(j) cha Kanuni za Uchaguzi wa Madiwani) na Kanuni za Wabunge na Rais,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, ni lazima vyama vione rasimu ya mwisho na kutoa maoni yao kwa kikao rasmi kabla haijawa kanuni ili kutoa uwanja sawa kwa wagombea.
CCM WATIA SHUBIRI
Aidha, katika kuzidi kuwatia kufuli wagombea upande wa CCM, wiki hii Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole alitangaza utaratibu mpya wa kupata wagombea wa ubunge na uwakilishi katika uchaguzi mkuu, baada ya kubaini uliotumika mwaka 2015 ulikuwa na upungufu.
Polepole alisema mchakato mpya utakaotumika Oktoba mwaka huu, umefuta utaratibu wa awali ambao mgombea ubunge alitakiwa kupita kata kwa kata na kwenye matawi kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni.
Kuhusu ubunge, vikao vitaanzia Kamati ya Siasa ya Wilaya, kisha Kamati ya Siasa ya Mkoa na baadaye Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa. Mchakato utaendelea kwenye Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa itakayojadili, kisha kuteua majina matatu ambayo yatakuwa ni siri kubwa.
“Yatafungwa na kuwekwa mhuri wa moto, kisha majina yale yatarejeshwa kwenye mkutano wa jimbo kwa maana ya wabunge na wawakilishi.
“Pale zitapigwa kura na wajumbe hao 1000… Mchakato utatengenezewa muhtasari… utafungwa kisha utaanza mchakato wa pili,” alisema na kuongeza kwamba taarifa hizo zitakwenda makao makuu ya CCM na kuanza mchakato wa kujadili hao watatu.
TAKUKURU
Wakati Polepole akianika namba mbili ambazo watu watawarekodi watu wanaotuhumiwa kutoa rushwa na kurusha taarifa zao kwenda kwenye chama, Takukuru imeahidi kuwabana vilivyo wagombea mwaka huu kuhakikisha hakuna vitendo vya rushwa vinavyoweza kujitokeza.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa Takukuru, Joseph Mwaiselo alisema mwaka huu agenda kuu ni kuhakikisha hakuna rushwa kwenye uchaguzi mkuu.
“Kwa sababu wanakuwa na ahadi ya cheo kwamba, ukinipatia hiki nitakupa hiki. Kuna wengine wamekuwa wakitumia usafiri kuwasafirisha wapiga kura, hawa tutawadhibiti,” alisema.
WACHAMBUZI WALONGA
Wakizungumza na IJUMAA kwa nyakati tofauti, baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa nchini, waliishauri NEC, kusikiliza madai ya wapinzani ili kuondoa kasoro zilizojitokeza na mwisho uchaguzi ufanyike kwa haki, uhuru na amani.
Licha ya kuunga mkono juhudi zinazotekelezwa na Takukuru, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa, alisema matarajio ya walio wengi yalikuwa ni kuona NEC inatoa kipaumbele kwa kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi uliopita.
“Kwa mfano, watu kutoona majina yao kwenye mbao za matangazo… ifafanue mwaka huu imejipanga vipi, pia ucheleweshwaji wa vifaa, hizi ni changamoto ambazo ni kero za uchaguzi, badala yake wanakuja na vipengele vya kubana wagombea.
“Ili kuondoa haya yote, utaratibu wao uwe shirikishi kwa sababu Watanzania tunahitaji uchaguzi huru na wa haki,” alisema.
Aidha, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala, naye alitoa wito kwa NEC kushirikisha vyama vya siasa katika kuondoa kasoro zilizojitokeza kwenye rasimu hizo.
“Pia vyama visiache kupiga kelele, kwa sababu huu ndio muda sahihi wa kuonesha mapungufu ili uchaguzi uwe huru,” alisema.
Wakati hayo yakijiri, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera alisema vyama vya siasa vimekuwa vikilalamika ili kutafuta huruma kwa sababu kila hatua vyama hivyo vilishirikishwa.
Pia Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria-NEC, Emmanuel Kawishe, aliwaomba viongozi wa siasa kutoa ushirikiano kwa kuwa tume itatenda haki kwa watu wote.
Stori: GABRIEL MUSHI, Ijumaa