×

Siri Nje! Aunt Kumnyang’anya Gari Wema

 

DAR: Mwanamama wa Bongo Movies, Aunt Ezekiel amezua gumzo kama lote mitandaoni baada ya kuposti picha akiwa amesimama kwenye gari aina ya Toyota Vanguard la rangi nyekundu ambalo mwaka jana alimzawadia rafiki yake, Wema Isaac Sepetu kiasi cha kuibua hisia kuwa huwenda amemnyang’anya, lakini sasa siri imefichuka.

 

Ilikuwa Septemba 28 (birthday ya Wema), mwaka jana pale Elements Club iliyopo Oysterbay jijini Dar ambapo Aunt alitangaza kumzawadia Wema gari hilo.

Hata hivyo, hivi karibuni, wawili hao walidaiwa kutibuana na kuvunjika kwa urafi wao huku sababu wakiijua wenyewe.

 

Baada ya kuposti picha hiyo, DJ wa Wasafi Classic Baby (WCB), Romy Jones alimuuliza kama ameshalichukua gari hilo ambalo alimpa Wema akiwa na maana kwamba huwenda amelichukua baada ya kugombana kwao.

 

Aunt alimjibu Romy kwa kujiamini kuwa ndiyo amelichukua.

Romy Jones: Umechukua na gari ulilomtunza?

Aunt: Ndiyo (alijibu Aunt na kusindikiza na emoj ya kucheka).

 

MASHABIKI SASA

Baada ya Aunt kujibu hivyo, baadhi ya mashabiki walianza kumponda Aunt kuwa, hakukuwa na sababu ya yeye kuweka hadharani kuwa amemnyang’anya shoga yake gari alilompa yeye mwenyewe kama zawadi.

 

“Mimi ndiyo maana huwa sipendi kuwa na marafiki kabisa maishani mwangu. Yaani kuna watu hata uwafanyie wema kiasi gani, bado kuna siku watakurudishia ubaya tu. Sasa kama gari alimpa yeye mwenyewe, kwa nini aanze kuweka tena hadharani? Wewe kama umekosana na mtu, ya nini kuanza kuanika hadi mambo yenu mliyokuwa mnayafanya?

 

“Mimi binafsi sioni sababu ya kuonesha kuwa amemnyang’anya gari alilompa, kwani sisi inatusaidia nini?” Alihoji shabiki huyo aliyefahamika kwa jina la Ester.

Wakati wengine wakimkosoa Aunt kwa kitendo alichokifanya, kuna ambao pia walimpongeza na kumwambia bora sasa na yeye aendelee na maisha yake.

 

“Jamani hata kama ningekuwa mimi ndiye Aunt, ningechukua zawadi yangu kwa huyo Wema. Halafu mimi sioni kama kuna shida yoyote yeye kupiga picha akiwa kwenye gari lake. Isitoshe, walikuwa wanamsema sana kipindi ana ushoga na huyo dada kuwa ni mnafki, sasa bora kila mtu ana maisha yake,” aliandika shabiki mwingine kwenye picha hiyo aliyefahamika kwa jina la Mrs Nurdin.

 

WEMA AZUNGUMZA

Gazeti la IJUMAA lilimtafuta Wema ili azungumzie ishu hiyo kwa upande wake ambapo alifunguka kuwa siyo kweli kwamba, Aunt alimzawadia gari, bali ni kitu ambacho kilipangwa.

 

“Lile gari Aunt hakunizawadia, ni kitu ambacho tulipanga ili ionekane vile, mwisho wa siku mimi na yeye hatuna shida, tupo sawa tu,” alisema Wema.

 

Aunt na Wema wamekuwa na ushosti wa kupanda na kushuka ambapo wamekuwa wakigombana mno kiasi cha kila mmoja kuapa kutomzika mwenzake, lakini baada ya muda hurejesha urafiki wao.

Stori: MEMORISE RICHARD, Ijumaa

Leave a Comment