×

Jembe AS Vita: Mimi Na Yanga! Mbona Fresh Tu

TUISILA Kisinda winga wa AS Vita ya DR Congo, amesema wazi kuwa wala haoni shida kujiunga na Yanga kwani ni klabu kubwa Afrika.Yanga kupitia Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, hivi karibuni alisema kuwa, watashusha vifaa vya maana katika usajili wa timu hiyo msimu ujao akiwemo winga tishio anayetoka katika ligi tano bora Afrika ambapo Congo ikiwa moja ya ligi hizo.

Akizungumza na Championi Jumamosi moja kwa moja kutoka DR Congo, Kisinda alisema tayari ameshafanya mazungumzo na Yanga na kama mambo yataenda sawa yupo tayari kujiunga na timu hiyo kuitumikia msimu ujao.

“Nilishafanya mazungumzo na Yanga juu ya wao kunisajili, kila kitu kipo vizuri japo mazungumzo hayajakamilika lakini naamini huko mbele yatakaa sawa kwa kuwa hata dirisha la usajili bado halijafunguliwa.

“Kujiunga Yanga sio tatizo kwangu kwani ni timu nzuri na kubwa kwa Afrika hivyo sitakuwa na kipingamizi kuichezea na baada ya kuhusishwa nayo nimeanza kuifuatilia mtandaoni nimegundua kuwa ni timu nzuri,” lilisema jembe hilo.

Kisinda mwenye umri wa miaka 20, anamudu kucheza nafasi za winga zote za upande wa kushoto na kulia, anakumbukwa zaidi baada ya kuifunga Simba bao moja katika ushindi wa 5-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika DR Congo mwaka jana.

Leave a Comment