Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli amewataka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) mkoani Mbeya kuwalipa wananchi milioni 20 kwaajili ya kuendeleza ujenzi wa Shule katika eneo la Kata ya Isongole, Kijiji cha Isyonje, Wilaya Rungwe, kwa Kaya 109 zilizozuiliwa kuendeleza maeneo hayo ambapo eneo hilo lilikuwa limependekezwa kujengwa mradi wa mzani wa kupima uzito wa magari.
Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kusikia malalamiko ya wananchi kupitia kipindi cha TBC1, Jambo Tanzania, jana asubuhi na ktoa maagizo hayo kwa njia ya simu wakati akiongea na wananchi wa Isyonje ambapo alimtuma mkuu wa mkoa huo Albert Chalamila kufuatili mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka minne kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2020, kati ya wananchi na TANROAD.
Akizungumza kwa njia ya simu Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila kusimamia zoezi hilo na kuwaacha wananchi waendeleze maeneo yao.
”Nimeona wananchi walikuwa wana lalamikia Tanroad kupitia wizara ya ujenzi wamechukua eneo lao kwaajili ya kujenga mzani, mpaka leo hawajawalipa fidia nikaona huo ni upumbavu waambie wananchi waendelee na shughuli zao, hakuna mtu yeyote atakaye wasumbua.
”Hao Tanroad wawaache wananchi waendelee kufanya kazi zao na kujenga nyumba zao na kama ni mzani utajengwa mahali kwingine wasiwe wanawasumbua watu, kwa mujibu wa sheria ya ardhi kifungu namba 4 na namba 5 kinasisitiza kulipa fidia kabla hujachukua ardhi,” alisema Magufuli.
Aidha, amewaomba radhi wananchi wa eneo hilo kwa kwa niaba ya watendaji wake kwa kuwacheleweshea maendeleo na kuwataka waendelee kufanya shughuli zao za kukuza uchumi wa Mkoa wa Mbeya na kuiagiza TANROADS kukipa kijiji hicho milioni 20 ili kiweze kumalizia ujenzi wa shule ya msingi inayojengwa.
Naye Mkuu wa mkoa wa Mbeya amesema “TANROAD kama mnataka kuchukua eneo la wananchi mjiandae mkiwa na hela ili wananchi wasisumbuke sasa kwakuwa mmejichelewesha, Rais wa nchi amesema wananchi wa eneo hili endeleni kujenga kulima na kufanya chochote”.
Kwa upande wa wananchi wa kata hiyo wamemshukuru Rais Magufuli kwa huruma yake na kusema kwa miaka mitatu wamesimamisha ujenzi na maendeleo yote katokana na mvutano wa eneo hilo.