
KABLA ya kuwachamba Wabongo wiki iliyopita, mwanamama Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ alichukuliwa kama mfano wa kuigwa kwa mabinti walio wengi.
Lakini baada ya hotuba yake hiyo iliyotafsiriwa kuwa ni matusi kwa Wabongo, mambo yamebadilika na kumuweka pabaya, sasa Zari aliyezaa watoto wawili na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, anashambuliwa kila kona.
Miongoni mwa wafuasi wake zaidi ya milioni saba kwenye ukurasa wake wa Instagram, wengi ni Wabongo ambao humfuatilia kujua mambo yake, hasa juu ya mafanikio aliyonayo na kwamba ni miongoni mwa wanawake waliozaa na Diamond ambaye ni kipenzi chao.
Wengine hupenda kutembelea kurasa zake za kijamii kuona mitindo ya mavazi ya bei mbaya, ili nao waweze kuendana na wakati kwani wanaamini ni mama wa kisasa.
Lakini pia wengine humfuatilia Zari kutokana na ujumbe wa kutamani mafanikio (inspirational statements), ambao huwa anaweka mara kwa mara kwenye kurasa zake.
Katika hotuba yake hiyo, Zari aliwachamba mno Wabongo kwa kuwaita washamba ambao wana chuki zisizokuwa na msingi.
Katika maelezo yake, Zari alisema kuwa, hata kama mtu akimchukia ni sawa kwani kama Watanzania wasipomfuatilia atafuatiliwa na mataifa mengine lukuki duniani ambao huwa wanamfuatilia.
Baada ya matusi yake hayo ndipo wakaibuka raia wenye hasira kali na kuanza kumshambulia kwa kumuita yale majina mabaya asiyoyapenda.
“Huyu kibibi kizee anajiona maisha ameyapatia kiasi hata cha kumkufuru Mungu, siyo sawa.
“Tuandamane, huyu bibi hawezi kutudharau Watanzania, hatuwezi kudhalilishwa na huyu mama na kutuita sisi maskini.
“Ni aibu Boss Lady kuchamba watu, hata akina Kim Kardashian na Oprah hawawezi kufanya ujinga kama wa kwake.
“Ukiona hivyo ujue pesa zimekata, ana hasira tele, mwambieni Diamond amtumie pesa angalau atulie.
“Mbona kama huyu dada analazimisha tumpende? Sijui anachoringia ni nini kwa sababu mali alizonazo ni za Ivan (aliyekuwa mumewe)!
“Au kuchezewa na viben’ten? Mimi ninamshauri huyu Tukinao aache kutafuta kiki kwa Watanzania.
“Jamani kwani King Bae aliishia wapi au alikufa? Anasema yeye ana pesa, anatembelea Range Rover, sasa mbona haolewi? Matokeo yake ameishia kuchezewa na vitoto kila siku,” ilisomeka sehemu fupi ya maoni lukuki ya Wabongo wakimshambulia mwanamama huyo.
Chanzo cha Zari kulipuka ni kufuatia baadhi ya kurasa za kijamii kudai kuwa anamfundisha mwanaye, Tiffah Dangote tabia mbaya ilihali bado ni mdogo.
Ilidaiwa kwamba, Zari amekuwa akimfundisha Tiffah maneno ya kikubwa ya kusema juu ya baba yake Diamond, kisha kumrekodi video na kutuma mitandaoni.
Hata hivyo, katika hotuba yake hiyo, Zari aliwashangaa Wabongo kwani mtoto ni wa kwake na hata akiharibika inawahusu nini?
STORI: HAPPYNESS MASUNGA, DAR