
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuanza rasmi kwa mchakato wa kutafuta wagombea katika kiti cha Urais, Wabunge, madiwani, wawakilishi na masheha huku kikiwaonya watia nia wote kutojihusisha na rushwa, kuwa wanyenyekevu na kufuata taratibu za chama hicho vinginevyo wataenguliwa.
Hayo yamesemwa leo leo Juni 12, 2020, na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi ndogo za CCM, Lumumba jijini Dar es salaam.
“Chama Cha Mapinduzi (CCM) tunapenda tufanye mambo yetu kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, sheria za nchi na kamuni tulizojiwekea ikiwemo kanuni za Uchaguzi na Uteuzi wa Wagombea.
“Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli amesema wagombea wa CCM wajitahmini, usigombee tu kwa sababu kuna uchaguzi mwaka huu, tunataka watu ambao watawawahisha Watanzania wanataka kwenye maendeleo.
“Tunawataka kuwapata viongozi wa CCM sio tu wawe na sababu mbili za kuwa na haki ya kugombea na kwa kuwa muda uchaguzi uchaguzi umefika, tunataka kuwapata viongozi ambao wana sababu zaidi ya hizo.
“Hivi karibuni tulikuwa na kikao na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa – TAKUKURU, nia yetu ni kuhakikisha rushwa haipati nafasi katika uchaguzi wa ndani wa chama chetu, tumefunga mitambo ya kudhibiti wavurugaji.”
“Watanzania wanajua, wanasubiri kauli ya CCM nani atakuwa wapi na wapi ili wabariki ila wavurugaji wanaweza kutia dosari. Wavurugaji hao tutawakata ndani ya CCM na tutapiga kampeni nzuri tutawakata kwenye uchaguzi mkuu.
“Sisi katika chama chetu hatutaki watu ambao wanaotaka uongozi kwa kujipeleka peleka, kwenye chama chetu uongozi hupewa, na tumekuwa na kiongozi Mkuu wa TAKUKURU kutusaidia kuwakamata wote watakaotoa rushwa wakisaka uongozi.
“Tunataka viongozi ambao wanaufahamu mwendokasi wa Rais Magufuli na wanaochukia rushwa pamoja na kujua Yale yote yanayomnyima usingizi kiongozi wetu Mkuu wa Chama, lakini pia tunataka watu ambao wanaojua kwamba Tanzania tumechelewa.
“Ratiba ya mchakato wa kumpata wagombea wa CCM wa Urais Tanzania inaanza June 15,2020 hadi June 30,2020 ambapo Watu watachukua na kurejesha fomu kisha baada ya hapo vikao vya uchujaji vitaanza.
”Julai 6 – 7, Kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya taifa ya CCM itakaa kwa ajili ya kuanza uchuchaji wa wagombea. Julai 8 ni Kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili na kisha Julai 9 ni Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu.”
”Julai 11 na 12 utaketi Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambao utakuwa na kazi ya kuchagua jina moja la mwanachama ambaye atasimama kuiwakilisha CCM katika majina matatu yatakayokuwa yamepitishwa na Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
“Wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kwa Tanzania Bara na Visiwani na Viti Maalum watachukua fomu kuanzia Julai 14 hadi 17, na mwisho wa kurudisha fomu ni Julai 17, 2020, saa 10 jioni.
”Watakaoomba nafasi za kugombea kiukweli wanatakiwa kujua maono ya kiongozi wa chama, Dkt Magufuli ili wakamsaidie katika kutekeleza majukumu yake huku wakijua wazi kuwa rushwa ni adui wa haki,” amesema Polepole.