
LICHA ya maambukizi ya Virusi vya Corona kuendelea kuitesa tasnia ya muziki nchini ikiwamo sekta mbalimbali, Msanii chipukizi wa muziki wa Bongo Fleva nchini, Zuhura Kopa ‘Zuchu’ amezidi kupasua kwa kujizolea umaarufu na mziki wake kukua kisanaa.
RISASI linachambua.Hilo limedhihirika baada ya msanii huyo machachari kuja kivingine kwa kupakua singo nyingine kali kuhusu Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyoamsha shangwe kwa wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
ZUCHU NI NANI
Zuchu ambaye ni mtoto wa Malkia wa Mipasho nchini, Khadija Omar Abdallah Kopa ‘Bi Khadja’, na muimbaji kindakindaki wa bendi ya CCM, – TOT, amefanikiwa ‘kutoboa’ katika kipindi ambacho maambukizi ya Virusi vya Corona yalikuwa yamezidi kushika kasi na kulazimu nchi nyingi ikiwamo Tanzania kusitisha mikusanyiko ikiwamo shughuli zote za starehe kama vile muziki.Aprili 8 mwaka huu, dunia ilianza kumtambua msanii huyo aliye chini ya lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) baada ya kuachia singo ya ‘Wana’ iliyopokelewa vema na mashabiki wa muziki nchini.

Mlimbwende huyo ambaye sasa ametimiza miezi mwili kwa umaarufu kwenye ‘gemu’, aliendelea kuachia ngoma kali kama vile Nisamehe, Raha, Kwaru na nyinginezo ambazo zote zilifanya vizuri.Aidha, akizungumza na gazeti dada la Risasi Jumamosi, Khadija alisema siri ya mafanikio ya mwanaye ni uvumilivu hasa ikizingatiwa ameanza muziki siku nyingi lakini cha kushangaza amekuja kukua na kupaa kimuziki katika kipindi hiki kigumu.“Subira huvuta heri, kwa sababu Zuchu ameimba muda mrefu sana. Kwa uwezo wa Mungu, sasa ndiyo ameanza kuwika. Ninachokijua kwa Zuchu ni mvumilivu sana na subira yake imemfikisha hapo alipo,” alisema Khadija.
VIONGOZI SERIKALI I WAMKUBALI
Aidha, kutokana na wimbo aliouachia wiki hii na kupigwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli, Zuchu amezidi kujizolea sifa kutoka kwa viongozi hao waandamizi wa serikali na CCM kwa ujumla.Katika kikao hicho ambacho mbali na kuongozwa na Rais Magufuli, pia walikuwamo viongozi wengine kama Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar; Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu; Kassim Majaliwa na Katibu Mkuu wa CCM; Dk. Bashiru Ally.
Viongozi wote ambao walioshiriki kikao hicho, walionekana kuwa na nyuso zenye furaha baada ya wimbo wa mrembo huyo kupigwa na kuwalazimu kunyanyuka kwenye viti vyao na kuanza kucheza.
Mapokeo ya wimbo huo yalionekana kuwakosha Watanzania wengi ambao wameweka kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kipande cha video za viongozi hao wakiucheza wimbo huo, jambo ambalo linaashiria kuwa msanii huyo amezidi kuonesha kipaji kwa sauti yake kali mbali na kubebwa na ‘WCB’.
MENEJA AZUNGUMZARISASI
lilizungumza na Meneja wa Zuchu, Said Fella ‘Mkubwa Fella’ ambaye alielezea furaha yake kuhusu ujio wa msanii huyo.“Zuchu ana miezi miwili tu kwenye gemu, tena alianza kuimba kipindi ambacho dunia nzima tulikuwa tunapitia kipindi kigumu cha Corona, Serikali ilizuia baadhi ya mambo kufanyika ili kujikinga na ugonjwa huo.“Lakini ndicho kipindi ambacho alifanya vizuri na mpaka sasa wakubwa wanamtambua na kutambua uwezo wake. Ni jambo la faraja kwetu, tumefurahi sana na niwaombe Watanzania, wazidi kutusapoti,” alisema.
STORI: MEMORISE RICHARD, RISASI