
MSHINDI wa gari mpya kupitia bahati nasibu ya Baba Lao au Jishindie Gari na Championi, Didas Mariki, anatarajia kukabidhiwa rasmi zawadi yake hivi karibuni katika ofisi za Global Publishers zilizopo Sinza Mori, Dar Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Usambazaji wa Global Publishers, Anthony Adam, alipokuwa anaeleza namna ambavyo utaratibu wa kutoa zawadi hizo utakavyotolewa kwa washindi wote ambao walipatikana kupitia droo hiyo kubwa iliyofanyika wiki iliyopita.
Adam alisema, mbali na Didas, kutakuwa na utaratibu mwingine wa kutoa zawadi kwa washindi sita ambao walijishindia shilingi 50,000, ambao walikuwa kama sehemu ya kusindikiza ushindi huo wa Didas.
Akielezea namna ambavyo mambo yatakuwa, Anthony alisema washindi wote saba watatakiwa kuja katika ofisi za Global Publishers ambapo watapokelewa na viongozi na wafanyakzazi wote wa Global Publishers, kisha washindi wote watapata nafasi ya kuzugumza na waandishi wakieleza namna ambavyo wamefanikiwa kuwa washindi.
Kisha baada ya hapo zoezi la kukabidhi zawadi hizo kwa washindi zitafuata. Anthony alisema: “Kesho Jumatano (leo), shughuli ya kukabidhi zawadi utafanyika. Washindi wote akiwemo Didas watakuja hapa ofisini kwetu, watapokelea na timu yote ya Global Publishers wakiwemo viongozi.

“Kisha watapata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari ikiwemo Global TV Online pamoja na magazeti yote ya Global Publishers, washindi watazungumza kidogo wakielezea bahati nasibu hiyo na namna ambavyo walifanikiwa kushinda, ndipo mwisho watakabidhiwa zawadi zao, yule wa gari ataondoka nalo na wale wa fedha nao itakuwa hivyohivyo,” alisema Anthony.
Marik, aliibuka mshindi wa jumla katika droo kubwa ya bahati nasibu hiyo iliyofanyika Jumatano ya wiki iliyopita maeneo ya Mabibo Sokoni.
Ambapo mbali na Marik kuna washindi wengine sita ambao walifanikiwa kushinda fedha taslimu shilingi 50,000.
Baada ya kushinda gari hilo Marik alisema Global Publishers imetimiza ndoto zake kwa wakati kwani wakati anaanza kucheza bahati nasibu hiyo alikuwa na malengo ya kushinda japo hakuwa na uhakika wa kama kweli angekuwa mshindi wa droo hiyo kubwa kwa mwaka huu.

Washindi wengine ni Khalifa Mwipawa, Seleman Ally Ruzegea, Maulid Ally, Msafiri Mawila ambao wote ni wakazi wa Dar. Wengine ni Mpoki Mwakyusa mkazi wa Mbeya na Kihiyo Hamisi mkazi wa Tanga.
Kabla ya kufanyika kwa droo hiyo juzi Jumatano kikosi cha Idara ya Usambazaji kilizunguka katika mitaa mbalimbali ya Dar kuinadi droo hiyo kubwa.
Bahati nasibu hiyo imetimiza lengo lake kwa kuwa madhumuni ya kuanzishwa kwa bahati nasibu hiyo ilikuwa ni kurudisha kidogo kinachopatikana kwa jamii ambayo ilikuwa inaisapoti Global Publishers kwa zaidi ya miaka 20.