
KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, amesema kuwa leo kikosi chake kitaingia uwanjani kwa lengo moja pekee la kupata ushindi na kamwe hawatawadharau wapinzani wao, Mbao FC.
Kauli hiyo aliitoa jana mara baada ya kumaliza mazoezi ya mwisho yaliyofanyika asubuhi kwenye Uwanja Simba Mo Arena uliopo Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Timu hizo leo zinatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo Simba inakamilisha ratiba baada ya kuwa mabingwa na kukabidhiwa kombe lao Jumatano iliyopita.
Akizungumza na Spoti Xtra, Sven alisema kuwa malengo yao ni kushinda kila mchezo uliopo mbele yao ili kuhakikisha wanaongeza idadi ya pointi msimu huu na kuweka rekodi

Hakuna mechi nyepesi kwetu, kuwafunga Yanga katika FA na kutangaza ubingwa mapema siyo sababu ya kwetu kucheza kwa dharau na badala yake tutaingia uwanjani kwa ajili ya kupata pointi tatu.“Malengo yetu katika mechi zilizosalia ni kushinda ili tuweke rekodi ya kuwa na pointi nyingi.
Watusamehe tu, hatutawaachia.“Tunafahamu haitakuwa rahisi kwetu kupata ushindi katika mchezo huu dhidi ya Mbao kutokana na wapinzani wetu kupambana wasishuke daraja,” alisema Sven.
Kwa upande wa nahodha wa timu hiyo, John Bocco ambaye yupo katika hatihati ya kucheza mchezo wa leo kutokana na jana kushindwa kufanya mazoezi kwa kile kilichoelezwa ni majeruhi, alisema kilichobaki sasa ni kuweka heshima na si kingine.