×

Wagombea Ubunge… Rekodi Tupu!

WAKATI kitendawili cha majina ya wagombea urais kupitia vyama mbalimbali vya siasa nchini kikiendelea kuteguliwa, kivumbi kimehamia kwenye nafasi ya ubunge ambayo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, imetajwa kuweka rekodi tano za kipekee. UWAZI linakupasha.

 

Kivumbi hicho kimeanza Julai 14, kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku makada wake wakichukua fomu za kuwania kuteuliwa kuwa mgombea ubunge kupitia chama hicho.

 

Aidha, mbali na CCM, tayari vyama vingine vikongwe ikiwamo Chadema, NCCR Mageuzi, ACT Wazalendo na CUF, navyo vimefungua dirisha kwa makada wake kuchukua fomu za kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya ubunge.

 

Uchaguzi wa mwaka huu, umevuta hisia za wanachama wengi kuwania nafasi za ubunge na udiwani, hali inayoelezwa na wachambuzi wa siasa kuwa, utakuwa uchaguzi wenye mabadiliko makubwa kutokana na upya wa sura za wagombea hao.

 

Wachambuzi hao walitaja rekodi tano ambazo zinabeba mabadiliko hayo katika uchaguzi mkuu kuwa ni pamoja na matumizi makubwa ya fedha kutopewa kipaumbele, utitiri wa watia nia majimboni, wanawake kujipima misuli kwenye majimbo badala ya kujikita kwenye viti maalumu huku wabunge waliobambwa kwa tuhuma za rushwa nao wakiweka rekodi ya kipekee kutokana na ‘style’ walizotumia.

 

RUSHWA YATIKISA

Mojawapo ya vitendo vilivyoanza kutikisa katika uchaguzi wa mwaka huu ni kuripotiwa kwa vitendo vya rushwa baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwa macho na kuwabamba wabunge wanaotetea nafasi zao kwa nyakati tofauti.

 

Baadhi ya watia nia wa CCM waliokamatwa kwa tuhuma za rushwa ni pamoja na Livingstone Lusinde (Mtera) ambapo TAKUKURU imechunguza na kutoa taarifa kuwa imekosa ushahidi wa tuhuma za rushwa kwa mgombea huyo, Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini) na Albert Obama (Buhigwe).

 

Tuhuma hizo zimewaweka kikaangoni watia nia hao, kutokana na msimamo wa CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu baada ya Katibu wake Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole kusema chama kimepokea taarifa za watia nia wanaotoa rushwa kutoka mikoa yote.

 

Polepole alisisitiza kuwa watu hao ambao majina yao yapo makao makuu, hawatapewa fursa ya kugombea uongozi kamwe.

 

MAWAZIRI WATOANA JASHO NA DAMU

Tofauti na chaguzi zilizopita, mawaziri wenye ubunge wa kuteuliwa, nao wamejitosa mapema kwenye uchaguzi mwaka huu hali iliyoamsha ari kwa wanataaluma wengine kutia nia ikiwamo viongozi wa dini kama vile Askofu Josephat Gwajima wa kanisa la Ufufuo na Uzima kupitia CCM.

 

Mawaziri waliotangaza kugombea mpaka sasa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi (Kilosna Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (Buhigwe).

 

Hata hivyo, baadhi ya mawaziri wengine nao wanaowania ubunge ni pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (Tanga Mjini), Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako (Kasulu) mkoani Kigoma.

 

UTITIRI WA WATIA NIA

Katika mojawapo ya jambo lililotia fora katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ni utitiri wa watia nia kupitia vyama mbalimbali nchini huku upande wa CCM ikiongoza kwa kuwa na rundo la wagombea hao.

 

Hali hiyo imedhihirika katika mikoa mbalimbali ikiwamo Mara yenye watia nia 167 wa CCM ilhali mkoa una majimbo 10, Kilimanjaro wenye majimbo tisa, hadi sasa kuna watia nia 124 kutoka CCM mbali na vyama vingine vya upinzani.

 

Hali hiyo, imeelezwa na wachambuzi akiwamo Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. George Kahangwa kuwa wingi huo ni dalili mojawapo ya nafasi ya ubunge kuonekana kuwa ni kazi rahisi.

 

Alisema pia hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, Watanzania hususani wasomi wengi, wameona daraja la kujikwamua kimaisha ni pamoja na kuwania ubunge au kujipitisha ili kupata uteuzi wa nafasi nyingine za kisiasa.

 

WANAWAKE WAJITOKEZA

Mabango mengi ya sura za walimbwende, yamekuwa yakisambaa katika mitandao ya kijamii na mbao za matangazo nchini… ambao wamenuia kuwania nafasi ya ubunge mwaka huu.

 

Hali hiyo ni tofauti na chaguzi zilizopita ambapo wanawake wengi walipimana ubavu katika nafasi za ubunge wa viti maalumu, lakini sasa watia nia hao kupitia vyama vya ACT Wazalendo, CUF, Chadema na CCM, wamejitokeza kwa wingi kuwania nafasi ya ubunge majimboni.

 

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wabunge wa majimbo, wanaume walikuwa 239 ilhali wanawake wakitajwa kutozidi 30 hali iliyodhihirisha kuwa Tanzania ina safari ndefu ya kufikia Azimio la Maputo la kufikisha idadi ya asilimia 50/50 ya wabunge ndani ya Bunge.

 

NI UBUNGE WA KIMYAKIMYA

Tofauti na chaguzi zilizopita, nafasi ya ubunge wa mwaka huu kwa upande wa CCM, imeonekana kuwa kaa la moto hasa baada ya chama hicho kuziba mianya yote ya rushwa.

 

Hali hiyo inatokana na chujio kali ambalo chama hicho imeliweka ambapo badala ya mbunge kutakiwa kupita kata kwa kata na kupigiwa kura za maoni, utaratibu wa sasa utahusisha Kamati ya Siasa ya Wilaya, Kamati ya Siasa ya Mkoa na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambazo zitawajadili waliochukua fomu na kutoa mapendekezo, kisha Kamati Kuu itateua majina matatu yatakayopelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa Jimbo.

 

Aidha, chujio hilo limedaiwa kupunguza matumizi makubwa ya fedha ambayo yalikuwa tishio kwa vijana wengi kujitokeza kuwania nafasi hiyo katika chaguzi zilizopita.

 

Vivyo hivyo kwa vyama vya upinzani, hali imeonekana kuwa sawa na CCM baada ya vijana wengi kujitokeza kuwania nafasi hiyo, bila kujali matumizi makubwa ya fedha ambayo awali yalikwamisha wagombea wengi wa nafasi hiyo.

 

WACHAMBUZI: WATANZANIA WAMEPATA ARI KUSHIRIKI SIASA

Aidha, kutokana na rekodi hizo, baadhi ya wachambuzi wa kisiasa akiwamo Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema utitiri huo wa wagombea ubunge, umedhihirisha kuwa sasa Watanzania wamepata ari ya kushiriki siasa.

 

Alisema pia wameonesha uzalendo kutaka kushika nafasi za kuisimamia nchi yao.

“Lakini mbali na hilo ubunge ni maslahi, ukiondoa wafanyabiashara wakubwa wanaofuata kwa kuwa na maisha mazuri, ni wanasiasa, kwa sababu wanapata mitaji ya kuanzisha biashara mbalimbali kupitia siasa,” alisema.

 

Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Dk. Kahangwa ambaye alisema mambo hayo yanachagiza uchaguzi wa mwaka huu kunoga zaidi hasa ikizingatiwa ongezeko la wasomi nalo limechangia kuwepo kwa wagombea wengi.

Leave a Comment