×

CCM Itaweza Kuruka Moto wa Vihunzi Hivi Kusini?

WAKATI moshi wa Uchaguzi Mkuu mwaka huu, ukizidi kufuka, yamkini mikoa ya Lindi na Mtwara sasa itakoleza moto wa uchaguzi huo ambao umeanza kunogeshwa na vuguvugu la utitiri wa wagombea ubunge.

 

Mkoa wa Mtwara ambao ulikuwa ngome ya CCM tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 uliandika historia mpya baada ya upinzani kubeba majimbo matatu kati ya 10.

 

Majimbo hayo ni Mtwara Mjini lililochukuliwa na Maftah Abdallah Nachuma (CUF), Cecil Mwambe kutoka Chadema alinyakua Ndanda ilihali Katani Ahmad Katani kutoka CUF akibeba Tandahimba.

 

Vivyo hivyo kwa upande wa mkoa wa Lindi ambao katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 ulitoa wabunge wawili wa upinzani kutoka CUF, Said Bungara (Kilwa Kusini) na Salum Barwany (Lindi mjini), katika uchaguzi mkuu wa 2015, Watanzania wameshuhudia ongezeko la jimbo moja la upinzani na kufanya mkoa huo kuwa na wabunge watatu wa upinzani kati ya nane.

Hayo yote yalijiri katika kipindi ambacho mikoa hiyo imetoka kwenye majeraha ya kupinga ujenzi wa bomba la gesi asili kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.

 

Mtifuano huo ulioibuka katika ungwe ya mwisho uongozi wa Jakaya Kikwete 2010 -2015, ulishuhudia hasira za wananchi walioandamana na kuchoma nyumba za viongozi waliokuwa wanaunga mkono ujenzi wa bomba hilo.

 

Waliopatwa na majeraha yaliyotokana na hasira za wananchi hao ni Mbunge Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM) ambapo nyumba yake ilichomwa kutokana na kadhia hiyo.

 

Licha ya hasira hizo kutulia baada ya nguvu ya vyombo vya dola kutumika, upepo wa aliyekuwa mgombea urais kutoka Chadema, Edward Lowassa ulikoleza moto wa nguvu ya upinzani katika mikoa hiyo ya Lindi ya Mtwara.

 

Lowassa alikuwa anaungwa mkono na vyama vitano vya upinzani vilivyounda umoja wao uliofahamika kwa jina la Ukawa.  Licha ya kwamba Lowassa hakushinda katika uchaguzi huo, hali ilikuwa tete kwa CCM baada ya kupokonywa majimbo manne katika uchaguzi huo.

 

Ingawa sasa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wenye sura tofauti na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa maana ya kwamba Rais John Magufuli anatetea kiti chake, huku akiwa anatumia nguvu kubwa kurudisha baadhi ya majimbo katika mikoa hiyo, tayari wananchi wa mikoa hiyo wamejeruhiwa tena katika kipindi cha 2015-2020.

 

Majeraha hayo yanatokana na anguko la mauzo ya mazao ya korosho, zao ambalo ndilo mkombozi kwa wananchi wa mikoa ya Kusini, kwamba maana ya kwamba Lindi, Mtwara na Ruvuma.

 

Umuhimu wa zao hilo la korosho si kwa mikoa ya kusini pekee kwani inakadiriwa kuwa huendesha maisha ya kaya zaidi ya 500,000 kama zao kuu la kibiashara katika wilaya zaidi ya 30 kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga.

 

Aidha, pamoja na mambo mengine, zao la korosho liligeuka kuwa kaa la moto baada ya kusabisha viongozi wa ngazi mbalimbali ikiwamo mawaziri kung’olewa katika nafasi zao.

 

Hayo yote yalitokea baada ya mwaka 2018 kuibuka mjadala mkali kuhusu mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2018 /2019 kuhusu zao hilo. Mapendekezo hayo yalikuwa pamoja na kuondolewa kwa ruzuku ya asilimia 65 iliyokuwa inaenda kwenye Mfuko wa Maendeleo wa Korosho na badala yake, ilielekezwa kwenye mfuko mkuu wa serikali.

 

Yalikuwa ni mabadiliko ya sheria ya matumizi ya fedha yaani (Finance Bill) ambayo baadhi ya wabunge na wananchi walikuwa hawayaungi mkono.

 

Mjadala huo kuhusu mapendekezo hayo ulionekana kugusa zaidi hisia za wabunge hasa wa mikoa ya kusini ambao moja kwa moja walitofautiana kuhusu mpango huo, lakini kwa nguvu ya Bunge ulifanikiwa kupita.

 

Aidha, Rais Magufuli naye aligongea nyundo baada ya kuwaeleza wazi kuwa asingefanya ajizi kuwatimua wabunge hao iwapo mpango huo ungekwama. Kwamba angewatimua wabunge 17 wa mikoa hiyo kutoka CCM iwapo wangeshindwa kuunga mkono mapendekezo hayo.

 

Hata hivyo, licha ya bei ya korosho kupanda na kushuka huku Rais Magufuli akiingilia kati na kuagiza serikali kununua korosho hizo, baadhi ya wananchi bado wana kilio cha kupatiwa malipo ya mazao yao hali inayotazamwa kukumbushia majeraha ya misukosuko ya zao hilo kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

 

Vivyo hivyo, kama ilivyokuwa kwa mvutano wa gesi asilia ambao baadaye hasira zilikolezwa na Lowasa, yamkini hasira za korosho zikakolezwa na Bernad Membe ambaye amehamia ACT Wazalendo wiki hii.

 

Vuguvugu la Membe lilianzia zaidi ya miaka miwili iliyopita, lakini Februari 28 mwaka huu, Kamati kuu ya CCM ilidai kuazimia kufukuza uanachama, kabla ya yeye mwenyewe kutangaza kurudisha kadi yake ya uanchama Julai 6 mwaka huu.

 

Hata hivyo, Membe ambaye anatarajiwa kupeperusha bendera ya ACT Wazalendo, anadaiwa kunogesha uchaguzi mkuu wa mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2015.

 

Tayari ameshaeleza wazi kuwa bila yeye, uchaguzi mkuu hauwezi kunoga na hiyo yote inatokana na historia nzito aliyojijengea kisiasa akiwa CCM.

 

Ujio wa Membe ACT Wazalendo na kusimama kwake kwenye nafasi ya urais, sasa kunatarajiwa kuzidisha mnyukano mkali baina ya CCM na upinzani hasa ikizingatiwa kuwa Membe ambaye alikuwa mbunge wa Mtama kabla ya kuamua kumuachia Nape Nnauye mwaka 2015-2020, analo kundi ndani ya CCM ambalo yamkini linamuunga mkono katika harakati zake.

 

Hii ndio inatajwa kuwa kitendawili katika majimbo ya mkoa huo, kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais na kuacha maswali kwa Watanzania kuwa je, CCM itaweza kuruka vihunzi hivyo katika mikoa hiyo ya kusini? Tusubiri tuone.

NA GABRIEL MUSHI

Leave a Comment