
DAKIKA chache mara baada ya Barcelona kupoteza mchezo juzi, nahodha wa timu hiyo, Lionel Messi hakuamua kujivunga wala kung’ata maneno, ni baada ya kuja juu na kudai kuwa wamefanya makosa mengi msimu huu.
Messi amekuja juu na kutoa kauli ambazo moja kwa moja zinaonyesha kumponda kocha wa timu yake, Quique Setien akionyesha kama ameshindwa kuifanya timu hiyo icheze vizuri na mwisho kupoteza ubingwa wa La Liga.
Barcelona ilipata kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Osasuna kwenye Uwanja wa Camp Nou, hivyo kusababisha Real Madrid itangaze ubingwa wa ligi hiyo.
Akionekana kuwa na hasira licha ya kufunga bao kwa timu yake, Messi alisema: “Mchezo huu unawakilisha kilichotokea msimu mzima, tumekuwa tukifanya makosa mengi na tumekuwa timu dhaifu.
“Madrid wamefanya kazi yao, wameshinda mechi zao kitu ambacho kinavutia, ni kama tumewasaidia kushinda ligi. Tumekuwa hovyo.“Tumepoteza mechi na taji kwa sababu ya makosa yetu na siyo kwa kuwa Madrid ni bora.
” Kwa kauli hizo inamaanisha kuwa ajira ya Quique ipo hatarini kwa kuwa ni nadra Messi kujitokeza na kutoa kauli hizo kwa timu yake