
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza rasmi kuwa tarehe 28, Oktoba, 2020 ambayo itakuwa ni siku ya UCHAGUZI MKUU itakuwa siku ya mapumziko.
Magufuli ametoa agizo hilo leo, tarehe 22, Julai 2020 wakati akizinduwa Jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ( NEC) eneo la Njedengwa jiini Dodoma ambalo limegharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 16.8 zilizookolewa wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Namshukuru Mwenyekiti wa Tume kwa kunialika. Ujenzi wa Ofisi hizi sio tu umependezesha mandhari bali umesogeza huduma kwa wadau wake. Hii itarahisishia wadau wake hususan wa vyama vya siasa kapata huduma zake.
“Naipongeza Tume kwa kuweza kujenga ofisi zetu za Makao Makuu hapa Dodoma. Tume hii hajawahi kuwa na jengo lake tangu 1993 ilipoanzishwa. Mmeingia kwenye vitabu vya historia. Naipongeza ofisi ya Waziri Mkuu wa kufuatilia kwa ukaribu ujenzi.
“Nawashukuru pia viongozi wa vyama vingine mliofika hapa (Prof. Lipumba, Mbatia na wengine) ndio maana nilipofika nikaona mmekaa mbali nikasema mje tukae pamoja huku, jengo hili ni letu, tutachukulia fomu hapa, hata mkisema hamchukui, tumekubali Magufuli umeshinda sawa tu.
”Nimeambiwa kampeni zitaanza Agosti 25 mpaka Oktoba 27, na uchaguzi utakuwa siku ya Jumatano, Oktoba 28, 2020. Siku ya uchaguzi Oktoba 28 itakuwa ni siku ya mapumziko, tutaitangaza rasmi. “Tufanye kampeni zetu kwa kujenga umoja wa taifa letu Tanzania, tunadi sera zetu na wananchi waweze kutupima kutokana na sera zetu, wasitupime kwa ajili ya matusi tunayo tukanana.
”Niviombe vyombo vya dola vituvumilie kidogo, ila visitumie nguvu, na sisi wanasiasa tusifanye mambo ambayo yatavifanya vyombo ya ulinzi vitumie nguvu, nawasihi tufanye kampeni za staha, tumtangulize Mungu mbele.
“Uchaguzi huu utakuwa huru sana, niwahakikishie ndugu zangu viongozi wa siasa, mimi ni mwenzenu tunajenga nyumba moja na nyumba hiyo tunayoijenga ni Tanzania nataka kuwathibitishia nitatoa ushirikiano mzuri sana kwa vyama vyote.”
“Napenda kuwasihi Tume katika Uchaguzi huu kusimamia Uchaguzi kwa kufuata Taratibu, Sheria na Kanuni za Uchaguzi. Narudia kuhimiza vyama vya siasa kushirikiana katika Uchaguzi huu na kujiepusha na vitendo vya vurugu. Vurugu hazijengi, zinabomoa,” amesema Magufuli.