×

JPM: Takukuru Mnanivuruga, Mnajenga Gereza? – Video

RAIS  John Magufuli ameeleza kutoridhishwa kwake na gharama zilizotumika katika ujenzi wa Jengo la ofisi za Ofisi Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Chamwino jijini Dodoma huku akieleza kuwa gharama za ujenzi huo ni kubwa ikilinganishwa na jengo lenyewe.

 

Magufuli amesema hayo leo, tarehe 22, Julai 2020, wakati akizinduzia wa jengo la TAKUKURU wilaya ya Chamwino jijini Dodoma ambalo limegharimu kiasi cha Tsh. Milioni 143.

 

“Hii ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria shughuli ya Takukuru tangu nimekuwa rais. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kazi kubwa ya kupambana na rushwa imefanyika na hili nalisema wazi, Takukuru kazi mmefanya. Takukuru imeweza kufungua jumla ya mashauri 2,256 ambapo mashauri 1,926 tayari yametolewa uamuzi na Serikali kufanikiwa kushinda mashauri 1,013 hii ni kazi ya Takukuru.

 

“Takukuru imeweza kuokoa kiasi cha Tsh bilioni 273.38, zikiwemo fedha walizokuwa wamedhulumiwa wakulima wa korosho, ufuta na maeneo mengine. Imetaifisha fedha taslimu Tsh. Milioni 899, Dola 1,191,651. Pia, Euro 4,301,399, nyumba nane zenye thamani ya Bilioni 11.6, magari matano ya Tsh Milioni 126. Imeweza kurudisha nyumba na majengo 98, mashamba 23, kampuni tatu na magahala 69, hongereni sana, kwa hakika ni mafanikio makubwa sana.

 

“Palipo na mazuri dosari hazikosi, zimezungumzwa. Salamu zenu hapa ni kung’ata ila mama Kuluthum aliwang’ata ninyi. Alikaa muda mrefu bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa sababu ya ‘connection’ aliyokuwa nayo ndani ya TAKUKURU. Rushwa ni mbaya sana ndugu zangu, na rushwa imetuchelewesha sana. Na nchi hii imepoteza mabilioni kwa sababu ya rushwa na wala rushwa walikuwa wafalme na walikuwa hawaguswi.

 

“TAKUKURU mmekuwa kama chombo ambacho hamguswi, na wale wachache wanaofanya mambo ambayo sio mazuri ndani y TAKUKURU mmekuwa hamuwafikishi mahakamani mnasema tu tumembana amerudisha, kwa nini asirudishe akiwa ndani kama wengine. TAKUKURU mnatakiwa kubadilika.

 

“Hii inaleta picha mbaya ndani ya TAKUKURU kwamba yakitokea mabaya ndani yenu hamshughulikiani. Hii inapoteza picha nzuri ya Taasisi. Mnatimiza wajibu wenu ila kuna asilimia kubwa hamtimizi wajibu wao. Mkurugenzi nataka ushughulikie hii.

 

“Huu haukuwa mradi wa kuja kufungua mimi wa milioni 143, lakini hata hivyo ni juu sana. Mimi nimejenga nyumba, mimi nimejenga nyumba na ninyi mmejenga. Na hili siwezi kuficha, ndiyo maana nimezunguka kuangalia. Nikasema hakuna kitu hapa tumeliwa. Nikazungumzie wapi, Ofisini? Hapa hapa ili Jenerali ujue. Nina uhakika kama umejenga nyumba huwezi kujenga hii kwa Milioni 143.

 

“Nimehesabu mabati ya upande huu, hayafiki 20. Nendeni mkahesabu! Sasa piga upande huu na ule na mwingine mara 4. TAKUKURU ng’ata! TAKUKURU ng’ata! Tanzania oyeee! Pamoja na kazi kubwa nzuri mnayofanya, lazima mjitathmini.

 

“Nilikuwa namuuliza Waziri Mkuu. Wewe unaweza kujenga nyumba hii kwa Milioni 143? Akasema mimi hapa kama Milioni 60. Nikaangalia mimi nyumbani nimejenga nyumba ukubwa kama huu Milioni 40. Nilikuwa naangalia hawa Wataalamu, nikasema ni wa Variation pia.

 

“Mmeokoa fedha nyingi, ningetamani niwape pesa za kujenga hizo kuta lakini si kwa gharama hiyo, nendeni mkakae tena. Inawezekana watu wanaokufanyia variation wasikupe gharama sahihi. Mtakaponiletea gharama ya kujenga ukuta ambayo siyo Bilioni 1 nitawapa kwa sababu TAKUKURU mnafanya kazi nzuri, na nina imani hiyo pesa haitazidi Tsh Milioni 500.

 

“Tulipoamua kuanzisha Makao Makuu Dodoma, kila Wizara ilipewa Bilioni kujenga Makao Makuu yake na ikamaliza kila kitu. Sasa Mgema akisifiwa Tembo hulitia maji. TAKUKURU msianze kuweka maji. Nataka Wafanyakazi hawa waishi kwa raha wanapoenda kwenye kazi zao waifanye kama Malaika. Anamkamata mla rushwa na kurudi kwakwe. TAKUKURU ni muhimu katika nchi hii.

 

“Natoa Bil mbili mkawajengee nyumba waishi kwa raha wakienda kufanya kazi wakaifanye kama Malaika, sio wanapanga kwenye nyumba za wala rushwa, Mkurugenzi usiwape hizo fedha hawa (Waliojenga nyumba za TAKUKURU), Hawa nimewashtukia mimi, hizi nyumba zijengwe na JKT, nilitegemea Boss wa TAKUKURU uniombe fedha za kujenga nyumba za wafanyakazi wa TAKUKURU Dodoma.

 

“TAKUKUru mnataka kunivuruga, kwanini unajenga ukuta wenye urefu wa mita 2? Ni Gereza? Ujue mtawekea vitu visivyo na msingi, Mimi urefu wangu ni Sentimita 168, Mita 1 na kitu. Wewe una mita ngapi? Sasa ukijenga ukuta mpaka ufike juu kama Gereza? Kwanini unaweka course 4 Ukiweka course 3 au 2 ukayalaza si inatimiza hitaji?

 

“Nimejenga najua ujenzi, usibishane. Najua ninachokisema. Unaweza kumdanganya Mkurugenzi. Nimekaa kwenye ujenzi kwa zaidi ya miaka 20. Inawezekana watu wako wanaokufanyia ‘variation’ wasikupe variation za kweli. Wewe (Mkurugenzi) si ulichukua law?

 

“Ukipiga hesabu, matofali yaliyoenda hapo unayajua! Unapima urefu wa nyumba unachukua tofali moja la nchi 6 unagawa kwa mita utakazopata. Sasa mbadilike na mabadiliko haya yawe ‘total change’. Mkianza na gharama za ujenzi na nimezisikia zamani kabla hata hujawa Mkurugenzi,” amesema Magufuli.

Leave a Comment