
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Sumbawanga, Julai 13 mwaka huu, ilitenda haki kwa kumhukumu Yustine Robart (35) kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe aitwaye Jackilina Lwiche na watoto wake wawili; Frenk Robart (4) na Elizabert Robart (6) na kisha kutumbukiza miili yao kisimani.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, David Mrango baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ambao ulikuwa na mashahidi wanne.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali, Lugano Mwasubira na mshtakiwa alikuwa akitetewa na wakili Patrick Mwakyusa.
Awali, katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Mwasubira aliiambia mahakama kuwa, mshitakiwa Yustine alitenda kosa hilo Agosti 5, 2013 majira ya saa nne usiku huko katika Kijiji cha Maji Moto, Wilaya ya Mlele, Mkoa wa Katavi.
Alidai kuwa, kabla ya kufanya mauaji hayo, mshtakiwa alikuwa na ugomvi na marehemu mke wake waliyekuwa wameishi naye kwa muda wa miaka sita.
Ilidaiwa kuwa, baada ya ugomvi huo, mume alimfukuza mke wake aondoke nyumbani kwake walipokuwa wakiishi naye pamoja na watoto wao watatu.
Mwasubira aliieleza Mahakama kuwa baada ya ugomvi huo kupita, ulizuka tena mgogoro wa kugawana vyombo vya ndani ambapo hata hivyo mshitakiwa alimruhusu marehemu kuchukua vyombo vyote isipokuwa jagi.

Inadaiwa kuwa, marehemu alikaidi agizo hilo kwa kulichukua jagi hilo na kulivunja kitendo ambacho kilimkasirisha mshtakiwa, ambapo alimpiga marehemu kisha akamtolea maneno kuwa atahakikisha anamfanyia kitu kibaya ambacho kitakuwa ni historia kwenye kijiji hicho cha Maji Moto.
Mwasubira alieleza kuwa, baada ya hapo marehemu hakuonekana pamoja na watoto wake watatu hadi mwanaye mdogo (2) alipopatikana akiwa hai kichakani akiwa ametelekezwa.
Inaelezwa kuwa, baada ya mtoto huyo kupatikana, wenzake wawili; Frank na Elizabert, walikutwa ndani ya kisima cha maji kilichokuwa umbali wa mita mia mbili kutoka kwenye nyumba waliokuwa wakiishi huku wakiwa wamefariki Dunia.
Mshtakiwa Yustine katika utetezi wake, aliomba Mahakama imuachie huru kwa kile alichodai kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kutoa ushahidi wa kuonyesha kuwa amehusika na mauaji hayo.
Madai hayo yalipingwa na mwanasheria wa Serikali, Mwasabira ambaye alidai kuwa, ushahidi wa mazingira unaonyesha kuwa, mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo.
Kabla ya kusoma hukumu hiyo, Jaji Mfawidhi Mrango alieleza kuwa, katika kesi hiyo, hakuna shahidi aliyethibitisha kwa ushahidi isipokuwa kesi hiyo imejengwa kwa ushahidi wa mazingira ambapo mahakama mbalimbali kama vile Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Afrika Mashariki, zimewahi kutoa maamuzi ya kesi kama hiyo kwa kuzingatia ushahidi wa mazingira.
Alisema miongoni mwa ushahidi wa mazingira uliotolewa kwenye kesi hiyo, unaomfanya mshtakiwa atiwe hatiani, ni kauli yake aliyoitoa kuwa atamfanyia marehemu kitu kibaya cha historia.
Kingine ni mshtakiwa hakuonesha juhudi za kuwatafuta mke na watoto wake baada ya kutoonekana na wala hakutoa taarifa popote kitu ambacho siyo cha kawaida kwa binadamu.
Kwa kuzingatia ushahidi wa mazingira, mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la kifungu cha sheria Namba 16 (1) cha kanuni ya adhabu kwa mshtakiwa atanyongwa hadi kufa kwa kosa la kuua watu watatu kwa kukusudia.
Baada ya hukumu hiyo, Yustine aliiomba Mahakama impatie nakala ya hukumu mapema ili aweze kukata rufaa.
STORI: WALTER MGULUCHUMA, KATAVI