×

Bilionea Laizer Apata Jiwe Jingine la Tanzanite

BILIONEA mpya wa madini aliyejizolea umaarufu nchini Tanzania, ambaye hivi karibuni aligeuka kuwa bilionea baada ya kupata mawe ya madini ya Tanzanite yenye thamani ya shiling bilioni 7.8, amegundua jiwe lingine la Tanzanite lenye thamani ya mabilioni kwa shilingi za Kitanzania.

 

Jiwe hilo lina uzito wa kilo 6.33, na thamani yake kamili inatarajiwa kutangazwa rasmi baada ya kuthamanishwa kwa jiwe hilo. Jiwe la sasa alilolipata Saniniu Kuryan Laizer ambaye ni mchimbaji madini mdogo,  linasemekana kuwa ni jiwe la pili kwa ukubwa kuwahi kupatikana katika machimbo ya madini hayo kaskazini mwa milima ya Mirelani.

 

Mwezi mmoja tu uliopita alipata madini ambapo moja lilikuwa na kilo 9.2 likiwa na thamani ya Sh. bilioni 4.5 na la pili lina kilo 5.8 lenye thamani ya shilingi bilioni 3.3. Serikali inatarajiwa kukabidhiwa jiwe la hivi karibuni kutoka kwa  Laizer ambapo inatarajiwa kuwa atakabidhiwa pesa kutokana na jiwe hilo.

 

Laizer mwenye umri wa miaka 52, ni mume wa wanawake wanne na amejaliwa watoto 30. Baada ya kupata madini hayo Bilionea Laizer aliyafikisha katika kituo cha utambuzi. Na serikali ya Tanzania iliyanunua  kwa thamani ya bilioni saba na milioni mia saba za Kitanzania.

 

Madini hayo yalikabidhiwa kwa serikali na Lazier ambaye ni mkazi wa Simanjiro akapatiwa fedha zake huko Mkoani Arusha kaskazini kwa Tanzania. Laizer alisema kuwa anapanga kujenga shule na kujenga kituo cha biashara kwao baada ya kupata pesa alizolipwa kutokana na mawe aliyoyapata awali.

 

Kupitia mtandao wa Twitter, Wizara ya Madini ya Tanzania ilimtambua Mtanzania huyo kama bilionea. Kwa mujibu wa wizara  hiyo, uzito huo hayajawahi kupatikana katika machimbo ya Tanzanite.

 

Tanzanite ni madini yanayopatikana  na kuchimbwa nchini Tanzania pekee. Mauzo ya madini hayo kwa mwaka 2019 duniani yalikuwa zaidi ya dola milioni 50 za Marekani. Yaligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania mnamo mwaka 1967, katika eneo dogo sana la madini la Mererani Hills, sehemu pekee ambayo madini hayo yanapatikana duniani.

Leave a Comment