×

Tuzo za VPL, Clatous Chama Kafunika Wote (Picha +Video)

CLATOUS Chama, mwamba wa Lusaka kwa msimu wa 2019/20, amekuwa kwenye moto ndani ya uwanja akiwapoteza wapinzani wake wote ambao ameingia nao kwenye mchakato wa tuzo ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

 

Tayari Chama msimu huu ametwaa tuzo mbili, ya kwanza ya Mchezaji Bora wa Kombe la Shirikisho na ya pili ni ile ya Mchezaji Bora wa SportPesa.

Usiku wa kuamkia leo, kwenye Ukumbi wa Mlimani City ulitarajiwa kuwa na sherehe za tuzo kwa wachezaji ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo jina la Chama anayekipiga ndani ya Simba lilikuwa kwenye vipengele viwili, cha kwanza ni kile cha mchezaji bora na cha pili ni cha kiungo bora.

 

Rekodi zinaonyesha kuwa, Chama amewapoteza wapinzani wake kwenye upande wa pasi za mwisho pamoja na mataji ambayo Chama amenyanyua kwa msimu wa 2019/20.

Chama amenyanyua mataji matatu akiwa na Simba, alianza kunyanyua taji la Ngao ya Jamii kisha taji la Ligi Kuu Bara na kumaliza na Kombe la Shirikisho huku akitimiza majukumu yake kwa kushirikiana na timu.

 

Kwa upande wa kiungo bora Chama alikuwa anashindana na Lukas Kikoti wa Namungo mwenye mabao manne na pasi saba za mabao akiwa amehusika kwenye mabao 11 kati ya 46 yaliyofungwa kwenye timu yake.

Mapinduzi Balama wa Yanga mwenye mabao matatu na pasi moja ya bao akiwa amehusika kwenye mabao manne kati ya 45 huku Chama akiwa ametoa pasi 10 za mabao na kutupia mabao mawili ndani ya ligi akihusika kwenye mabao 12 kati ya 78.

 

Kipengele kingine ilikuwa ni upande wa mchezaji bora alikuwa akipambana na Nicolas Wadada wa Azam FC mwenye pasi saba za mabao na alifunga bao moja pamoja Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union mwenye bao moja.

Kwa rekodi ndani ya ligi pamoja na washindani wake, Chama ameonekana kuwafunika wote hata akipewa tuzo zote mbili hakuna ubaya kwani rekodi zinambeba.

Leave a Comment