KLABU ya Azam FC jana Jumapili, ilizindua tamasha lake la Azam Festival katika shughuli iliyofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, zoezi lililoambatana na kutambulisha jezi zao mpya.
Uzinduzi wa tamasha hilo, ulihudhuriwa na mamia ya wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu hiyo, huku Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao, akiwa kama mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo ambaye pia alihusika katika kuzindua na kutambulisha jezi mpya za timu hiyo.
Azam Festival ni tamasha lililoandaliwa na uongozi wa Azam FC, lengo lake kubwa likiwa ni kutoa nafasi kwa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kukutana na kujivunia uwepo wa klabu hiyo ikiwemo kuukaribisha msimu ujao wa ligi na mashindano ya kimataifa.
Shughuli na michezo mbalimbali ilifanyika jana Jumapili katika Uwanja wa Azam Complex. Vikundi vya Jogging kutoka Temeke, vilipata nafasi ya kufanya mazoezi na kufuatiwa na mechi za mpira wa miguu.
Sherehe za tamasha hilo zitahitimishwa Agosti 23 kwa Azam FC kutambulisha wachezaji wake wote na kucheza mchezo wa kirafiki na timu ambayo itawekwa wazi hapo baadaye.
ISSA LIPONDA, Dar es Salaam
