MSEMAJI wa chama cha upinzani nchini Urusi kiitwacho Russia of the Future, ameeleza kuwa kiongozi wa chama hicho ambaye pia ni mwanaharakati mashuhuri nchini humo, Alexei Navalny (pichani), amenyweshwa sumu iliyowekwa kwenye chai, na sasa yuko katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) baada ya kupoteza fahamu.
Navalny (44) alianza kujihisi vibaya wakati akirejea kwa ndege jijini Moscow kutoka mji wa Tosk, Siberia, jambo lililolazima ndege hiyo kutua kwa dharura huko Omsk ambapo msemaji wake, Yarmysh alisema Navalny alikuwa amekunywa chai tu kabla ya kuanza safari hiyo.
“Tunahisi Alexei aliwekewa sumu kwenye chai, kwani ndicho kitu pekee alichokunywa asubuhi. Madaktari wanasema sumu hiyo iliyeyuka haraka katika chai hiyo ya moto,” alisemaYarmysh.
Mwanasiasa huyo bado yuko hospitali akiwa hajitambui, kwa mujibu wa daktari mkuu wa hospitali hiyo, Alexander Murakhovsky, aliyenukuliwa na shirika la habari la TASS la nchini Urusi.


