MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia chama cha ACT Wazalendo, Bernard Membe, amewakaribisha ndani ya chama hicho wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliokatwa katika kuwania ubunge.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Membe ameandika” “Uteuzi wa CCM uliofanywa umenifurahisha sana, nawapongeza wote waliobahatika kuteuliwa, lakini kubwa zaidi nawapa pole wale wote waliokatwa kwa sababu ya kuwa karibu nami, hiyo ni baraka siyo balaa, karibuni mjiunge na ACT- Wazalendo haraka ili safari iendelee”.
Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, alijiunga na ACT Wazalendo Julai 7, 2020, baada ya kufukuzwa ndani ya CCM amesema, waliokatwa ndani ya chama hicho kuwania kugombea ubunge wajiunge na ACT Wazalendo.
Jana Alhamisi, CCM ilitangaza majina ya walioteuliwa kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 28, 2020, huku ikishuhudia zaidi ya waliokuwa wabunge 70 wakishindwa kutetea nafasi zao.
