The House of Favourite Newspapers

Kauli ya Tizeba Kwa Shigongo Yashangaza -Video

0

KAULI ya mbunge wa Buchosa aliyemaliza muda wake, Charles Tizeba, akimpigia chapuo mgombea aliyepitishwa mwenzake  Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo, imewashangaza wengi na kumsifia kwamba ameonyesha ukomavu wake wa kisiasa na kwa chama chake.

 

Tizeba alienguliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Shigongo kupitishwa baada ya wawili hao kufungana katika kura za maoni,  jambo ambalo lilihisiwa na wengi lingemfanya kada huyo wa chama ‘kununa’.

 

“Mambo makubwa yaliyofanyika Buchosa kwa miaka mitano tunasema asante sana Mheshimiwa  Rais; umetupatia hospitali ya wilaya, sasa kazi yako Shigongo tekeleza, songa mbele. Wananchi wa Buchosa tumpe kura Shigongo, wafuasi wa Tizeba mliokuwa mnanuna ole wenu niwaisikie!” alisema Tizeba wakati akizungumza kwenye kampeni za mgombea wa urais, John Magufuli, huko Bukokwa, Sengerema, jana.

 

Kinyume na matarajio  ya wengi Tizeba aliibuka na kauli hiyo ya kushangaza ambayo ilizua mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii.

 

Hata hivyo,  kwa upande wake Shigongo alisema kuwa atakuwa mbunge wa watu wote waliomuunga mkono na wale wasiomuunga mkono na kusema kuwa kilichotokea kwenye mchakato wa kura za maoni ilikuwa ni demokrasia na wala siyo uadui.

 

“Ndugu zangu wana Buchosa nawaomba tuwe kitu kimoja, makundi tuyavunje ili tupate ushindi wa kishindo, baadaye tulete maendeleo kwenye jimbo letu.

 

“Hatuwezi kushinda tukiwa tumegawanyika, hatutapata maendeleo tukibaguana,” alisema Shigongo.

 

Tizeba na Shigongo walifungana kwenye kura za maoni ndani ya CCM kwa kila mmoja kupata kura 354 ambapo Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa Kamati Kuu alisema waliengua jina la Tizeba baada ya kubaini kuwa alikuwa mmoja kati ya wajumbe waliokuwa na sifa za kupiga kura hivyo kupata nafasi ya kujipigia.

 

“Katika kura hizo walizofungana ukiitoa kura moja aliyojipigia Tizeba mshindi anakuwa ni Shigongo, hii ndiyo kanuni tuliyotumia,” alisema Rais Magufuli wakati akihutubia mkutano wa kampeni katika kijiji cha Bukokwa,  Mwanza, jana.

Leave A Reply