×

Magufuli: Nimealikwa Kwenda Ulaya, Siendi – Video

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa kazi ya urais si nyepesi, kwani ana uzoefu wa miaka 25 katika siasa na amejifunza mengi kwa kipindi hicho huku akiyasoma na kuyatambua matatizo na shida za Watanzania.

 

Magufuli amesema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa Chato katika kampenzi zake alizofanya kwenye Uwanja wa Mazaina na kuongeza kuwa haoni mtu mwingine anayegombea urais anaweza kufanya mambo aliyoyafanya hata robo.

 

 “Dkt. Kalemani amefanya kazi kubwa ya kusambaza umeme vijijini, limekuja Bomba la Mafuta tunajua tulichokifanya, ujenzi umeanza, leo kuna mtu atasema Kalemani tulikuwa hatumuoni ulitaka aje nyumbani kwako? Nilishangaa watu 60 kujitokeza, nikasema wataisoma namba.

 

“Wakati Mimi mnanichagua kuwa Mbunge Jimbo hili lilikuwa linaitwa Biharamulo Mashariki haikuwa wilaya. Miaka mitano iliyopita Tanzania ilikuwa na uchumi wa chini lakini sasa dunia nzima inajua kuwa Tanzania iko uchumi wa kati, jipongezeni.

 

“Daraja la Busisi tuliloanza kulijenga ndio litakuwa daraja refu zaidi Afrika Mashariki. Litakuwa na urefu wa kilomita 3.2 na ujenzi wake unagharimu bilioni 700. Hakuna mtu alitegemea tutapata fedha sisi wenyewe za ujenzi. Haya ni maajabu.

 

“Kuongoza ni kutoa lengo, kuongoza ni kuongozwa pia kuongoza panahitaji karama, kuongoza panahitaji upendo, kuongoza ni tofauti na kuzungumza kwamba nitafanya hivi, nitafanya hivi.

 

“Uongozi ni kutoa sadaka, nimeamua kutoa maisha yangu ya uongozi kama sadaka kwa Watanzania, hii kazi ndugu zangu ni ngumu lakini ninaweza kuifanya tena kwa miaka mitano. Tunapochagua mtu hatuchagui sura, mimi sura yangu mbaya kweli lakini tunachotaka ni maendeleo yanayo-focus watu.

 

“Wapo watu mawazo yao ni kupata fedha kwa wafadhili kila kitu wafadhili, unadhani wafadhili hawataki kuishi huko kwao, wanatoa wapi pesa? Atafute hela yake kuja kukupa wewe? Ukiletewa hela yoyote na wafadhili ujue utalipa mara mbili au mara tatu, mtu anasimama ameshiba amevimba mashavu anasema atafuta kodi, hata Biblia imesema vya Kaisari mpeni Kaisari na vya Mungu mpeni Mungu, hakuna vya bure.

 

“Mahusiano sio kwenda Ulaya, nataka mahusiano mazuri kwanza na Watanzania ambao wamenipigia kura, hata sasa kuna mwaliko wa kwenda kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa, siendi, nitatuma Balozi wa Tanzania anayetuwakilisha huko Marekani, ndiyo kazi ya Balozi.

 

“Mtakumbuka wananchi walivyouawa kule Kibiti, askari zaid ya kumi, hata kutoka Chato kwenda Biharamulo zamani ilikuwa mpaka usindikizwe na polisi. Vyombo vya usalama vimefanya kazi kubwa kuilinda amani ya nchi yetu, nchi haiwezi kuogopa majambazi.

 

“Mzee Mkapa alininadi kwenye kiwanja hiki hiki, ndio maana napomfikiria Mzee Mkapa moyo unaniuma sana, kwa sababu ndiye aliyeniokota huku jalalani, maana kuna msemo siku hizi mtu akipata kazi anaitwa ameokotwa jalalani na Magufuli,” amesema Magufuli.

 

Leave a Comment