ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Ikabidi yule mtaalam aanze kunitafuta kwa kutumia ramani alizokuwa akizijua yeye mpaka akafanikiwa kujua sehemu niliyokuwa nimehamishiwa ambapo kulikuwa na ulinzi makali uliokuwa umeimarishwa katika kila kona, hali iliyompa ugumu mtaalam kushindwa kunitafuta.
SASA ENDELEA…
Baada ya kufanikiwa kujua sehemu nilipo, mtaalam alichukua timu yake aliyokuwa nayo ambayo ni wale ndugu zangu pamoja na mwenyekiti wa kijiji chetu na kuanza kunitafuta tena huku akitumia ufundi wake kwa jinsi alivyokuwa akiaminiwa.
Sasa wakiwa njiani wanakuja pale kwenye ile ngome niliyokuwepo, pia wakuu wa pale wakawa wameshatambua kwamba kuna watu wanakuja kwa ajili ya kuninasua na ili wasiharibu kazi yao ikabidi taratibu za kunitoa zianze kufanyika tena kwa haraka sana.
Kusema ukweli ilikuwa hali ya taharuki kubwa, ngome yote ilikuwa kama imetikisika. Hofu ilitanda kwani ilionekana kwamba, kitendo cha yule mtaalam na ndugu zangu kufanikiwa kunitoa ni aibu kwa kambi ya misukule na ni ushindi mkubwa kwa watu wanaopambana na vitendo vya wachukua misukule. Kwa hiyo siku hiyo hawakuweza kuninasua.
Kwa hiyo kushindwa kwa mtaalam kunitoa ngomeni kulisitisha imani ya mimi kuja kuishi duniani tena. Ilifika mahali nilihisi kama nimeridhika na maisha ya kule kwa sababu ya kuzoeana na misukule mingine. Ikumbukwe kwamba, ndani ya ngome sikuwa mtu wa kusemasema mbele ya viongozi.
Basi, maisha yakawa yanaendelea huku nikishuhudia wenzangu, wageni kwa wenyeji wakikatwa ndimi zao bila huruma kwa lengo la kuwapumbaza.
Naamini inakumbukwa kwamba, nyuma nilishasema, mtu yeyote aliyechukuliwa msukule akishakatwa ulimi tu, akili inahama. Anakuwa mbumbu au zezeta. Yaani uwezo wa kutambua mambo kama binadamu unapotea ghafla.
Hapa naomba niseme tena kidogo kwamba, zile ndimi licha ya kukatwa kwa lengo la kumpumbaza mlengwa, lakini pia zinatumika kama firigisi za kuku na kilikuwa ni chakula maalum kwa ajili ya maofisa tu. Ninaposema maofisa tu namaanisha viongozi wa ngazi za juu wa kule kwenye ngome.
Hapa ijulikane wazi kwamba, ndani ya mikikimikiki yote hiyo, tayari nilikuwa nimeshatimiza miaka mitatu tangu nilipofariki dunia huku duniani na wale ndugu zangu walikuwa wakiendelea kunitafuta bila kukata tamaa. Waliamini ipo siku moja watanipata.
Siku moja baada ya kula chakula cha asubuhi, tulitakiwa kwenda shambani kulima kwa mujibu wa ratiba lakini wakati tumebeba majembe tayari kwa kutoka, ghafla ilipigwa kengele ya dharura, hivyo zoezi la kwenda shambani likasitishwa na maofisa wakakaa kikao kizito.
Mimi sikujua kilikuwa kikao kinachohusu nini, lakini nilishangaa nikiamriwa nitolewe haraka sana katika ile ngome. Haukupita muda mrefu wakaletwa askari pamoja na wanajeshi ambao walikuwa ni ndege hawa warukao.
Ndege hao walikuwa bundi ambao ndiyo walikuwa na cheo cha wanajeshi na popo ambao walikuwa kama askari polisi.
Basi, nikatolewa pale kwa mwendo wa ajabu, yaani ulikuwa wa mwendo wa kasi mimi nikiwa natembea huku wale ndege wakiwa wamenizunguka kwa juu lakini nilikuwa nina nguvu fulani kiasi kwamba nilikuwa sichoki kwa mwendo ule.
Niliendelea kutembea chini ya ulinzi huo mpaka tukafika mahali nikajikuta niko juu ya jiwe refu na wakati huo nilikuwa nimechoka sana huku wale ndege wakiwa wamenizonga pande zote. Ghafla ndege mmoja akatua kwenye bega langu. Tena nakumbuka siku hiyo nilikuwa kifua wazi.
Baada ya kutua, makucha yake yakaniumiza, nikahisi maumivu makali mno, nikampiga yule ndege kwa mkono wangu, akaanguka chini na kufa palepale. Wale ndege wengine waliokuwa bado wananizonga walikusanyika. Wakanipa adhabu ya kunipiga makofi, ikafika mahali nikaona naweza kuanguka na kufa ikabidi nitafute sehemu yenye kabonde nilale.
Nikapata sehemu ya hivyo nikalala kweli. Lakini akili ilikuwa haijui nini hasa maana ya kuingizwa mle. Nilihisi huenda kitendo cha kumuua yule ndege kilichangia. Ghafla nikahisi kuna mkono wa mtu unanivuta kutoka pale kwenye bonde, nilishtuka sana, lakini baadaye nikajikuta namwuliza yule mtu kwamba hivi wewe hauna akili? Yule mtu hakunijibu, nikasema huoni kama hili jiwe ni refu sana na nikidondoka chini naweza kufa?
Baada ya kutamka maneno hayo, ghafla ikaja mikono mingi sana, kama ya maelfu ya watu, ikanisukuma na kujikuta nimetumbukia kwenye pango kubwa. Nilijiuliza maswali mengi nini maana yake?
Niliichekecha sana akili yangu lakini sikuwa najua kitu. Tena na lile giza lililokuwemo mle ndani ya pango nikajisemea moyoni bora nilipokuwa kwenye lile jiwe kabla ya kusukumwa.
Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Ndugu Zangu Walinichukua Msukule.