MENEJA wa Msanii wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ Saidi Fella maarufu kama Mkubwa Fella, anayegombea Udiwani Kata ya Kilungule iliyopo Mbagala Jijini Dar, Jumamosi iliyopita alisababisha mafuriko ya umati wa watu wakati akizindua kampeni za kukiwania kiti hicho kwa msimu wake wa pili. Uzinduzi wa kampeni hizo, ulifanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Martin Lumbanga, vilivyopo Kata ya Kilungule.
Katika uzinduzi huo, kabla ya Fella kupanda jukwaani, zilitangulia burudani kutoka kwa wasanii wa Bongo Fleva, Taarab na ngoma za asili. Upande wa Bongo Fleva, kulikuwa na wasanii mbalimbali akiwemo Lavalava, taarab walikuwepo Prince Amigo, Aisha Vuvuzela na Mishi Zele.
Wasanii wa ngoma ya Kindengereko, nao waliingia kwenye viwanja hivyo na kufanya yao ili kunogesha mambo kabla ya kumpisha Mkubwa Fella kumwaga sera zake na kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena kwenye kiti hicho cha kuiongoza kata hiyo.
Baada ya burudani hizo, Mkubwa Fella alipanda jukwaani na kuwaomba kura wananchi wa kata hiyo, huku akiwakumbushia mengi aliyoyafanya kipindi chake kinachomaliza muda wake. Miongoni mwa mambo aliyotaja kuyafanya kwenye kata hiyo, ni pamoja na kuchimba visima sehemu mbalimbali kwenye kata hiyo iliyokuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.
Fella akiendelea kuwakumbushia wananchi hao, aliwaeleza alivyopambania elimu kwenye kata hiyo na kufanikiwa kujenga Shule ya Martin Lumbanga walipofanyia uzinduzi huo. Fella alizitaja barabara kadhaa kwenye kata hiyo ambazo zilikamilishwa kwa usimamizi wake na kuahidi kufanya mengine zaidi ya hayo. Sera hizo zilisababisha umati huo uliofurika, kupiga mayowe ya kumshangilia.
“Tunakujua Mkubwaaa… lazima tukuchague tenaaa”. Walisikika baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo. Sambamba na Mkubwa Fella, wengine waliopanda jukwaani hapo kuomba kura, ni pamoja na mgombea ubunge wa Jimbo la Mbagala, Abdallah Chaurembo na madiwani wote wa jimbo hilo.
HABARI; RICHARD BUKOS, UWAZI
