×

Young Killer, H.Baba Kuisimamisha Buchosa leo

ITAKUWA balaa pale ambapo wasanii wakubwa wa Bongo Fleva, Young Killer na H.Baba watakapopishana jukwaani leo Ijumaa kutoa burudani ya kumsindikiza mgombea Ubunge wa Jimbo la Buchosa, Eric James Shigongo atakapozindua kampeni zake kwenye Uwanja wa Nyakaliro, uliopo Buchosa, Mwanza.

 

Mbali na Young Killer na H.Baba, wapo pia Joel Lwaga, Paul Clement, Ronna Max, Jane Misso na Dox Flavour, ambao wote kwa pamoja watafanya balaa lao kwenye jukwaa hilo wakati mgombea huyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) atapozungumza mbele ya wananchi na wanachama wa CCM kutoka Jimbo la Buchosa na maeneo mengine jirani na eneo hilo kwenye shughuli itakayoanza saa 3:00 Asubuhi hadi 12:00 Jioni.

 

Shigongo anatarajia kufungua kampeni zake leo Ijumaa, kunadi na kutangaza nia, dhamira na sera zake kwa wananchi wa Buchosa na kuwapa sababu za kwa nini wanatakiwa kumchagua yeye, kuliongoza jimbo hilo kwa miaka mitano.

 

Mgeni rasmi katika ufunguzi huo anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania na Mgombe Ubunge Jimbo la Ruangwa, Lindi, Kassim Majaliwa.

 

Uzinduzi huo wa kampeni ulitakiwa kufanyika tangu Septemba 11, lakini ulisogezwa mbele kwa sababu ya ziara ya Rais John Magufuli na mgombea urais kupitia CCM mkoani humo.Hivyo uzinduzi ukapangwa ufanyike Septemba 24, lakini Waziri Majaliwa alipendekeza ifanyike Septemba 25 kwa sababu ndiyo tarehe ambayo naye ilimtaka kuwa na ziara mkoani humo.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Makoye Augustine alisema kila kitu juu ya maandalizi ya uzinduzi huo yamekaa sawa, baada ya kupigwa kalenda nyingi kipindi cha nyuma na hatimaye mambo yameiva.

 

“Timu yetu imetimia na ipo vizuri kabisa, kila kitu kimekaa mahala pake, wasanii wote watakuwepo, wageni na wagombea wote wa udiwani kutoka kwenye Jimbo la Buchosa watakuwepo pia, kwa hiyo kazi itabaki kwa wananchi wenyewe ambao bila shaka watajitokeza kwa wingi,” alisema Makoye.

 

Championi lilisonga mbele na kumtafuta Young Killer hili kujua amejiandaje kwa shoo ambapo alisema: “Unajua Mwanza mimi ndiyo nyumbani, halafu Shigongo ni mtu ambaye namkubali sana tangu nikiwa dogo kutokana na kazi zake. Hivyo kupata nafasi kama hii ni kama kutimiza ndoto nzuri.

 

“Shoo itakuwa kali sana, nitaimba hadi Kisukuma, kwa sababu nitakuwa na Wasukuma wenzangu, lazima nitambe nikiwa kwetu, hivyo watu waje kwa wingi uwanjani kusikiliza sera na kupata burudani ya michano mikali lakini pia kupata nyimbo za kiroho kutoka kwa kina Joel Lwaga,” alisema Young Killer.

 

Kampeni hizo, baada ya kuzinduliwa leo pale Nyakaliro, zitazunguka katika kata zote 21 kutoka kwenye Jimbo la Buchosa na kupita kwenye maeneo mengine kama Nyehunge, Bupandwa, Kasisa, Nyakasasi, Bukokwa, Bugoro, Kalebezo, Irenza, Iligamba, Katwe, Maisoma Kisiwani, Bulyaheke na kwenye kata zingine sambamba na vijiji.

 

Katika moja ya sera za Shigongo alisema kuwa, anahitaji kuboresha miundombinu ya barabara, umeme, afya, maji na elimu ambavyo kwa muda mrefu vimeshindwa kupatiwa ufumbuzi kiasi ambacho wananchi wamekuwa wakiishi maisha duni kwa kukosa kiongozi bora.

Leave a Comment