
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeibuka kinara kwenye Maonesho ya Madini na Teknolojia yaliyomalizika mwishoni mwa wiki mkoani Geita ambapo taasisi hiyo imefanikiwa kutwaa jumla ya tuzo tatu ikiwemo tuzo ya mshindi wa kwanza kwa taasisi za kifedha na benki zilizoshiriki kwenye maonesho hayo.

Benki hiyo pia ilifanikiwa kutwaa tuzo ya Mdhamini Mkuu wa maonesho hayo kwa taasisi za fedha huku pia ikifanikiwa kuibuka mshindi wa tatu wa jumla katika maonesho hayo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hizo na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Uwekezaji Bi Angellah Kairuki aliemuwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkurugenzi wa Idara ya wateja binafsi, benki ya NBC Makao Makuu Bw Elibariki Masuke alisema tuzo hizo tatu zinaakisi mafanikio makubwa ambayo benki hiyo imeyapata kupitia maonesho hayo.

“Kimsingi tuzo hizi tatu zinaakisi mafanikio makubwa ambayo benki ya NBC tumeweza kuyapata kupitia maonesho haya ikiwemo kuendesha program mbalimbali za mafunzo kwa wadau takribani 600 wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji wadogo na wajasiriamali.’’ Alisema

Aliongeza kuwa mkakati wa benki hiyo baada ya maonesho hayo ni kutekeleza kwa vitendo masuala muhimu iliyoahidi kuyafanya kwa kushirikiana na wadau hao ili kuboresha zaidi sekta hiyo.
Katika maonesho hayo benki hiyo pia iliendesha huduma za kibenki ikiwemo kufungua akaunti mpya kwa wateja, kuendesha kliniki ya biashara ambayo ilisaidia kukusanya maoni ya wadau wa sekta ya madini zaidi ya 150 ambao walikutanishwa na taasisi mbalimbali za serikali.

Aidha kupitia makongamano mbalimbali benki hiyo iliwawawezesha wadau wa sekta ya madini kubadilishana mawazo baina yao wenyewe lakini pia baina yao na mamlaka mbalimbali za serikali ikiwemo Wizara ya Madini, TRA, NEMC, SIDO na TANTRADE, TABWA, OSHA,GST na NSSF.
NA MWANDISHI WETU, GEITA