×

Kiba Apewa Silaha Kumkabili Mondi

BAADA ya kuibuka kwa vuta ni’kuvute mpya kati ya mastaa wakubwa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au ‘Mondi’, hatimaye Kiba amepewa silaha ya kumkabili mwenzake huyo.

 

Kiba na Mondi wamekuwa kwenye ushindani mkali kwa kuachia nyimbo zao kali ambazo zimekuwa zikiwasha moto mitaani, kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kusikiliza, kutazama, kuuza na kununua muziki.

 

Hivi karibuni King Kiba ametikisa na kukiwasha tena kwa mara nyingine, baada ya kuachia wimbo mkali unaokwenda kwa jina la Mediocre ambao hadi leo Jumamosi umetazamwa zaidi ya mara milioni 1.8 ndani ya wiki  moja, huku Mondi akitisha na audio ya Wimbo wa Ongeza ikiwa na watazamaji zaidi ya milioni 1.1 ndani ya wiki mbili katika Mtandao wa YouTube.

 

Kwa upande wake, Wimbo wa Cheche ambao Mondi ameshirikishwa na memba wa lebo yake ya Wasafi Classic Baby (WCB), Zuhura Othman ‘Zuchu’ ulikuwa umetazamwa zaidi ya mara milioni tatu kwa wiki moja.

 

Nyimbo za Mediocre na Cheche kwa sasa zimekuwa kwenye mchuano mkali kwa kupigania trending namba moja, ambapo Mondi na Zuchu wameshikilia mpini na kubaki kileleni kwa muda wa wiki moja sasa.

 

MNAJIMU AFUNGUKA

Kutokana na kuwepo kwa ushindani huo kati ya mastaa hao wakubwa wa Bongo Fleva, mnajimu na mtabiri maarufu Afrika Mashariki, Maalim Hassan Yahya Hussein amefunguka na kumpa mbinu Kiba za kuzidi kupanda na kumkabili Mondi.

 

Akizungumzia kinyota, Maalim amesema kuwa, Kiba anatakiwa ajiongeze na kujitengeneza ili kumkabili hasimu wake ambaye wamekuwa kwenye ushindani mkubwa wa kimuziki.

 

“Kiba bila kujitengeneza anaweza kuanguka kimuziki, maana hata Harmonize amemshusha kwa sasa, zamani kwenye ushindani tulizoea kusikia Kiba na Diamond, lakini kwa sasa ni Harmonize.

 

“Labda mambo ya dini yamemkaa sana maana yule amesoma sana chuo cha dini.

“Mwanzoni kabisa alikuwa akishika namba moja, baadaye akaja kushuka hadi tatu, kwa hilo akizubaa hata huyu msanii mpya ambaye anakuja vizuri kwa sasa Zuchu, naye atamdondosha,” alisema Maalim na kusisitiza kwamba, mbali na kushika dini, lakini silaha kubwa kwa Kiba ni kujiongeza kwa namna nyingine kama anavyofanya Diamond.

 

MASHABIKI WATAMBIANA

Timu mbili za mastaa hawa, zimekuwa zikishindana mitandaoni, ambapo kila moja imekuwa ikiegemea upande mmoja wa msanii wake na kutambiana kwa kazi kali zinazotoka kwenye platform (mitandao) zote za kupakua muziki. “Kiba ni kaka tu hata akitulia anaachia ngoma, ona alivyokiwasha tena,” aliandika shabiki mmoja wa Kiba.

 

Kwa upande mwingine, mashabiki wa Mondi walionesha kumsapoti na kusema kuwa Kiba ameweka mashairi ya kumsema hasimu wake.

“Kwenye wimbo huo ukisikiliza vizuri, utaona jinsi gani Kiba alivyomkejeli Mondi, lakini hata hivyo Mondi bado anatikisa na kubaki kileleni siku zote hata wamfanye nini,” aliandika shabiki wa timu Mondi.

 

TUJIKUMBUSHE

Kiba na Mondi walikuwa karibu sana na baadaye wakaingia kwenye bifu zito kwa miaka sasa, kiasi cha kuonekana ni mahasimu wakubwa, kwani hata wakutanapo, hawana stori zaidi ya kila mtu kufanya yake.
STORI: HAPPYNESS MASUNGA NA KHADIJA BAKARI, DAR

Leave a Comment