×

Shigongo Bega kwa Bega na Wananchi!

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Buchosa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo James ameahidi kushirikiana bega kwa bega na wananchi katika kuleta maendeleo jimboni Buchosa.

 

Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake katika Jimbo la Buchosa, uliofanyika Kata ya Nyakaliro Halmashauri ya Buchosa.

 

Alisema kuwa, atatumia maarifa yake ambayo amekuwa akiyatumia kufundisha maelfu ya watu takriban nchi nzima, namna ya kutoka hatua moja kwenda nyingine kiuchumi.

“Ni muda sasa umefika tushirikiane ili jimbo letu lipate maendeleo na wananchi wanatamani kupata maendeleo kutoka kwetu,” alisema Shigongo.

 

Katika uzinduzi huo, Shigongo alisema kuwa, atahakikisha anaboresha miundombinu ya elimu shuleni ili watoto wapate elimu bora kama wanavyopata watoto wengine kwa kushirikiana na wananchi.

“Katika kuboresha elimu, mkinichagua nitahakikisha walimu wanapata motisha pamoja na wanafunzi wanaofanya vizuri kuwapatia zawadi, hii itasaidia ufaulu kupanda katika shule zetu za msingi na sekondari,” alisema.

Sambamba na elimu, pia alisema ataboresha huduma ya afya, miundombinu ya barabara ili wananchi wa jimbo la Buchosa wapate huduma bora pamoja na kusafiri kwa urahisi katika maji na nchi kavu.

 

Aidha, katika sekta ya kilimo na uvuvi alisema kuwa, kwenye uongozi wake endapo atachaguliwa, atahakikisha wananchi wa Buchosa wanalima kilimo cha kisasa pamoja na kuweka ulinzi madhubuti kwa wavuvi ili kupambana na maharamia wanaowadhuru wavuvi katika Ziwa Victoria, ili wananchi wa jimbo hilo wanufaike na kuondokana na umaskini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Marco Makoye aliwataka WanaBuchosa na Sengerema kwa ujumla wao, wawapatie kura wagombea Ubunge wa Majimbo ya Sengerema na Buchosa, pamoja na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuri ili kuleta maendeleo ya haraka.

STORI: DENIS MTIMA, DAR

Leave a Comment