MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Buchosa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo James, jana Jumapili, Oktoba 11, 2020, aliendelea kutikisa kwa nguvu kwenye kampeni zake katika Kata ya Iligamba, ambapo alifanya mikutano mitatu ya hadhara kuzungumza na wananchi wa kata hiyo.
Katika mikutano yake Shigongo ameendelea kumwaga sera zake ili wananchi wa Jimbo la Buchosa na kata hizo waweze kumpatia fursa ya kuwatumikia na kutatua changamoto zao, ambazo ni pamoja na tatizo la umeme katika baadhi ya maeneo, ubovu wa miundombinu ya barabara, uvuvi na suala la afya na elimu.
Akizungumza na wakazi wa kata hiyo, Shigongo amewaomba wananchi wote kumpigia kura nyingi mgombea urais kupitia CCM, John Magufuli, madiwani wa CCM pamoja na yeye kwenye nafasi ya ubunge ili waweze kutimiza ndoto za wananchi hao kwa wakati, kwani amejipanga kuboresha maeneo yote huku kwenye barabara akiahidi kununua katapila lake kwa ajili ya kuboresha barabara.
“Ndugu zangu nafahamu wengi wetu tuna changamoto nyingi za kichumi, ambazo zinatokana na ubovu wa baadhi ya miundombinu ya barabara, sekta ya afya, elimu na nishati ya umeme, hivyo naomba mnitume ili nije kutatua matatizo hayo kwa haraka.
“Siombi ubunge ili nitajirike kwa maana mshahara wake ni mdogo tu, jambo ambalo mimi nimeamua kuja kuwatumikia ili siku moja nikiondoka kila mmoja wenu abaki anakumbuka kuwa aliwahi kuwepo mtu aliitwa Shigongo, alifanya makubwa, naomba mtambue kuwa mimi ninaguswa sana na matatizo yenu ndugu zangu, hivyo itapendeza mkinichagua Oktoba 28, mwaka huu ili nikamalize kero zenu.
“Mimi ni mzaliwa wa jimbo hili katika Kijiji cha Katwe, kisha wazazi wangu kuhamia Mwangika na baadaye Bupandwamhela ambapo ndipo naishi, hivyo nimeguswa kuja kutatua matatizo ya jimbo hili ambayo yamekuwa yakinikwaza hata mimi kwa miaka mingi, ushawishi wangu umetokana na ubora wa CCM ya Magufuli ambayo imeleta mabadiliko makubwa, hivyo niwaombe mtuchague kwa pamoja ili tuboreshe yote yanayotusumbua,” alisema Shigongo.
Shigongo anaendelea na kampeni zake jimboni Buchosa akinadi sera za chama chake cha CCM pamoja na kuwaomba ridhaa wananchi ili wawachague viongozi wa CCM kuanzia kiti cha urais, ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.
View this post on Instagram






