Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu wafanyabiashara wanne wakiwemo raia wawili wa kigeni kulipa fidia ya shilingi Milioni kumi na sita kwa kosa la kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA hasara ya zaidi ya shilingi milioni kumi na sita.
Washitakiwa hao ni, Alven Swai, Godluck Macha wakazi wa Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam, wengine ni, Betha Ngunyi na Frolennce Wanjira wakazi wa Nairobi Nchini Kenya.
Washtakiwa hao wamehukumiwa kulipa fidia hiyo baada ya kuingia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini DPP.
Shauri hilo limesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Yusto Ruboroga ambapo washitakiwa Betha Ngunyi na Frolennce Wanjira wametakiwa pia kulipa faini Shilingi laki tano kila mmoja kwa kosa la kuishi nchini bila vibali maalumu vinavyotambulika kisheria.
Aidha, mahakama hiyo pia imetaifisha vifaa vya kielektroniki ikiwemo kompyuta mbili za mpakato, mashine mbili za kuunganisha internet na laini za simu zaidi ya hamsini ambazo washitakiwa hao wanadaiwa kuzitimia kutenda uhalifu wa kimtandao.
Washitakiwa hao wamefanikiwa kulipa faini hiyo baada ya kufikia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini DPP baada ya kukiri makosa yao.
