×

Hatimaye Ndoa Ya Lulu na Majizo Yatangazwa Kanisa

MAPAMBIO ya ndoa ya staa wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mchumba’ke, Francis Siza ‘Majizo’, yameimbwa mpaka basi, angalau sasa dalili za rekodi kuwekwa sawa zimeonekana, Risasi Mchanganyiko linakuhabarisha.

 

Fukuto la jambo hilo kutimia, lilikolea mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye mitandao ya kijamii, ambapo Majizo kupitia ukurasa wake wa Instagram, alitupia picha akiwa na Lulu na kuandika:“Comments zihusu ukumbi gani utatosha!”

Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mchumba’ke, Francis Siza ‘Majizo’.

Posti hiyo iliamsha utamu uliokuwa umekata wa ndoa yao, ambayo imesubiriwa zaidi ya miaka mitatu na kuonekana kama usanii, ambapo wengi walianza kuhisi kuna jema linakuja nyuma ya wachumba hao wazoefu Bongo.

Mara paaap, Jumapili iliyopita ndani ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Andrea Bahari Beach jijini Dar es Salaam, ndoa ya wawili hao ilitangazwa kwenye ibada na watu kuishia kusema “Hatimaye.

”Kwa mujibu wa taratibu za Kanisa Katoliki kabla ndoa yoyote haijafungwa, ni sharti itangazwe kwa majuma matatu mfululizo.

 

Tangazo la ndoa ya Lulu na Majizo Jumapili iliyopita, ni la kwanza na kwamba, baada ya wiki mbili zijazo, wawili hao watakuwa tayari kuunganishwa kimwili na kuwa kitu kimoja.

 

Lulu na Majizo wamekuwa wakijiiba kimapenzi kwa muda mrefu, ambapo Septemba 2018, uchumba wao uliingia kwenye hatua ya kuvikana pete ya uchumba, kisha wakatulia zao.

 

Tangu hapo, hawaoani hawaoani, zimekuwa nyingi hadi kufikia hatua ya uzushi kuenea kwenye mitandao ya kijamii kwamba, Majizo ameamua kubadili gia angani na kuachana na staa huyo wa filamu.

 

Mara nyingi wawili hao, wamekuwa kama wanacheza na akili za watu, kwa kuacha kila lisemwalo juu yao mitandaoni na kwenye vyombo vya habari lipite, pasipo majibu yao kuhusu ndoa yao hadi tangazo halisi la Jumapili lilipotoka hadharani.

 

Hata hivyo, Risasi Mchanganyiko lilipowatafuta wachumba hao kwa nyakati tofauti ili kujua ni lini watafunga ndoa, hawakupatikana.Mmoja kati ya watu wa karibu nao, aliliambia gazeti hili kuwa:“Ndoa itafungwa mwezi wa kumi na moja, kama una lingine kuhusu masuala ya sherehe yao, watafute wenyewe,” alisema mtu huyo kwa sharti la kutotajwa jina.

 

Kabla ya Lulu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Majizo, staa huyo wa filamu alikuwa akitoka na nguli wa Filamu Bongo, marehemu Steven Kanumba, ambaye baadaye aliingia matatani kwa kuhusika na kifo chake.Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 kwa kile kinachotajwa kuwa, ni baada ya kutokea ugomvi kati yake na Lulu, ambaye alikwenda nyumbani kwa Kanumba usiku wa tukio.

 

Kufuatia kifo cha Kanumba, Lulu aliingia kwenye msukosuko wa kisheria, hadi Novemba 2017 alipokutwa na hatia ya kuua bila kukusudia na mahakama kumfunga jela miaka miwili.Hata hivyo, Mei 12, 2018, staa huyo alitoka jela na kutakiwa kumalizia kifungo chake kwa kufanya kazi za kijamii kwa amri ya Mahakama Kuu.

 

Kufuatia mauaji hayo ya Kanumba, Lulu alijikuta kwenye mgogoro na mama mzazi wa msanii huyo wa kiume bora Bongo, Flora Mtegoa.

 

Mara kadhaa mama Kanumba alinukuliwa akimlaani Lulu, kwa kile alichokuwa akikitaja kuwa ni kuhusika kwake na kifo cha mwanaye na baadaye kujitenga naye.

 

Hata hivyo, mama huyo amekuwa na vipindi vya ‘kuwaka’ na ‘kupoa’ kwa Lulu, ambapo juzi mwandishi wetu alipomtafuta na kumuuliza anatoa neno gani kwa Lulu ambaye anatarajia kufunga ndoa na Majizo hivi karibuni, alisema:“Namtakia kila la heri, nimeshamalizana naye, sina tatizo, kama kuna kiapo nilishakiondoa zamani na kumsamehe kabisa,” alisema mama Kanumba alipozungumza na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita kwa njia ya simu.

MWANDISHI WETU, RISASI

AUNTY EZEKIEL Afunguka SIRI ya MIMBA Yake, Kuhusu KUSAH – “NI MWANAUME, SIONI SHIDA”

Leave a Comment