×

Baba Aliyefiwa Familia ya Watu Watano – Video

BABA mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Edward Jeremiah Katemi, amejikuta katika wakati mgumu, baada ya familia yake ya watu watano, ambao ni mke wake Jacqueline Frank, mdogo wake Ester Katemi na watoto wake Edwin (10) Evon pamoja na Edson (6) kufariki dunia kwa ajali ya moto huko Pugu Mnadani jijini Dar.

 

Akizungumza na RISASI Jumamosi, Katemi alisema tukio hilo la kusikitisha, lilitokea wiki iliyopita usiku, wakati familia hiyo ikiwa imelala.

Alisema chanzo cha moto huo, kinadaiwa ni hitilafu ya umeme uliolipuka ghafla na kusababisha nyumba hiyo kuwaka moto.

 

“Umeme ulikuwa umekatika, uliporudi, ulirudi kwa kasi, ndipo ilipotokea shoti na nyumba yangu ilipoanza kuteketea kwa moto, uliosababisha mauti kwa familia yangu iliyokuwa ndani.

“Wakati umeme unarudi, sikuwepo nyumbani, lakini wakati nyumba inaanza kuungua, tayari nilikuwa nimeshafika getini.

 

“Nilikuwa nimeenda kwenye mihangaiko yangu, baada ya kutoka nikawa nimerudi mida ya saa 3:57 usiku.

“Wakati nipo getini, nikawa nabisha hodi ili nifunguliwe niingie ndani, ndipo umeme uliporudi kisha soketi zikatoa cheche, shoti kubwa ikapiga ikabidi nishuke kwenye gari na kuingia ndani, nikaona nyumba inaungua kwa ndani.

 

“Nikaanza kupiga kelele kuomba msaada watu wakaja, kwa bahati nzuri mvua ilikuwa imenyesha, hivyo maji yalikuwa mengi tukaanza kumwagia ndani.

 

“Baada ya kumwagia maji kwa muda mrefu, tulifanikiwa kuuzima moto, mwisho ikabidi tutoboe ukuta ili tuingie ndani, tulipoingia kwanza chumba cha watoto, tukakuta watoto wawili ambao ni Edwin na Edson, tayari walikuwa wameshakata pumzi.

 

“Baada ya hapo, tukaingia kwenye chumba change, nikamkuta mke wangu kipenzi Jacqueline akiwa na mwanangu Evon wakiwa wamedondoka chooni, ndipo tulipowatoa nje.

“Mwisho tukaingia kwenye chumba cha mdogo wangu naye tukamtoa, kwa pamoja tukawapeleka kwenye hospitali ya Nguvu Kazi iliyopo Chanika.

 

“Baada ya kufika huko, kwa bahati mbaya wakawa wamefariki, Mungu akisaidia Jumamosi (leo) tunaweza tukasafirisha miili kwenda Sengerema Mwanza kwa mazishi,” alisema.

Akizungumzia taratibu za mazishi hayo Baba wa familia hiyo, alisema watasafirisha miili hiyo kwenda Kijiji cha Sukuma kilichopo kata ya Bukokwa – Buchosa Sengerema mkoani Mwanza na leo ndiyo mazishi ya marehemu hao.

 

MAJIRANI WAFUNGUKA

Wakizungumza na RISASI Jumamosi baadhi ya majirani wa eneo hilo akiwamo jirani mmoja aliyejitambulisha kwa jina la mama Mashamba, alielezea kusikitishwa na tukio hilo.

 

“Nilipata taarifa saa 4:30 usiku, nilishtuka sana kwa sababu sio kitu nilichokitegemea, inauma sana kupoteza ndugu watano kwa wakati mmoja, lakini ndiyo hivyo kazi ya Mungu haina makosa. Nawaombea marehemu wapumzike kwa amani,” alisema Mashamba.

STORI: MEMORISE RICHARD

 

Leave a Comment