
RAIS wa Chama cha Waongoza Ndege Tanzania (TACC), Shukuru Nziku, amesema, ndege-nyuki (drones) ni miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo waongoza ndege na hiyo inahatarisha usalama wa ndege angani.
Amesema ‘drones’ hurahisisha kazi kama ujenzi wa miundombinu na upigaji picha za kawaida katika maeneo mbalimbali lakini wanashindwa kuzifuatilia kutokana na kutoonekana zikiwa angani.
Ametoa wito kwa watengenezaji wa drone na watafiti kubuni njia itakayoweza kuunganisha vifaa hivyo na mamlaka za anga ili kuepusha hatari inayoweza kujitokeza.
Nziku amesema kwa nchi ya Australia, kifaa hicho kimesababisha majanga kwa ndege hivyo wanafanya jitihada za namna ya kuzifanya zitumike pasipo kuleta madhara. Hapa nchini drone zimeshamiri kwa kuwa ni nyenzo muhimu katika kupiga picha na video kwenye zama hizi za sayansi na teknolojia.