×

Simba Sasa ni Ushindi tu

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba, leo Jumatatu wana kazi ya kusaka pointi tatu mbele ya Ruvu Shooting ambayo nayo ni timu ya wajeda kama ilivyokuwa kwa Prisons ambao waliwachezesha gwaride kwa kuwafunga bao 1-0, Uwanja wa Nelson Mandela, Alhamisi ya wiki iliyopita.

 

Kazi kubwa kwa Simba inayonolewa na Sven Vandenbroeck raia wa Ubelgiji ni kwenye kusaka rekodi ya kuendeleza ubabe wao mbele ya Ruvu Shooting inayonolewa na Charles Mkwasa.

 

Rekodi zinaonesha kuwa tangu, msimu wa 2010/11, timu hizo zimekutana mara 18, Simba imeshinda mechi 16 na sare mbili. Haijapoteza.

 

Jumla ya mabao 51 yamefungwa ikiwa ni wastani wa bao moja kila baada ya dakika 31. Katika mabao hayo, Simba imefunga 43, huku Ruvu Shooting ikifunga nane.

 

REKODI ZINAIBEBA SIMBA

Kwenye mechi nane za mwisho za misimu minne nyuma ambazo timu hizi zimekutana, Simba imefanikiwa kushinda mechi saba, sare ikiwa moja.

 

Matokeo yalikuwa hivi;

2016/17 (Simba 2-1 Ruvu Shooting, Shooting 0-1 Simba),

2017/18 (Simba 7-0 Ruvu Shooting, Ruvu Shooting 0-3 Simba).

2018/19 (Ruvu Shooting 0-5 Simba, Simba2-0 Ruvu Shooting),

2019/20 (Ruvu Shooting 0-3 Simba, Simba 1-1 Ruvu Shooting).

 

UBORA WA SIMBA UPO HAPA

Safu ya ushambuliaji ya Simba, ndipo ubora wao ulipo kwani imefunga mabao 14 kwenye mechi sita. Safu ya ulinzi imeruhusu mabao matatu.

 

MKWASA TATIZO KWA SIMBA

Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Mkwasa, amekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Simba msimu uliopita akiwa anainoa Yanga ambapo mchezo wa kwanza alifanikiwa kupindua meza kibabe kwenye sare ya mabao 2-2, na raundi ya pili akiwa kocha msaidizi wa kikosi hicho, Yanga ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.

 

TATIZO LA RUVU

Ruvu Shooting kumekuwa na ugumu kwenye safu yao ya ushambuliaji ambapo hadi sasa kikosi hicho kimefunga mabao matatu kwenye mechi saba, huku kikiruhusu mabao manne.

 

WATAKAOKOSEKANA

Simba inatarajiwa kuwakosa Meddie Kagere, John Bocco, Chris Mugalu, Shomari Kapombe, Gerson Fraga na Ibrahim Ame ambao watakuwa nje ya uwanja kutokana na kuuguza majeraha.Kwa upande wa Ruvu Shooting, ofisa habari wa timu hiyo, Masau Bwire, amesema kikosi chao wote wapo fiti.

 

KAGERE ASHUSHA PRESHA

Akizungumzia kuhusu maendeleo yake, Kagere alisema: “Kwa sasa naendelea vizuri na matibabu kufuatia majeraha niliyoyapata kwenye mchezo wetu dhidi ya JKT Tanzania kule Dodoma, baada ya kufanyiwa vipimo madaktari walifikia uamuzi wa kunipumzisha kwa muda.

 

“Kuhusu ni lini nitarejea uwanjani hilo ni suala lililo chini ya timu ya madaktari kwani hapo awali nilipewa wiki tatu za kupumzika na nimekuwa nikifanyiwa vipimo vya mara kwa mara ili kujua kasi ya uponaji wangu na ni imani yangu kuwa nitarejea uwanjani hivi karibuni.”

LUNYAMADZO MLYUKA NA HUSSEIN MSOLEKA

 

Leave a Comment