UMOJA wa Mataifa umetoa wito kwa Tanzania kuhakikisha uchaguzi mkuu wa kesho Jumatano, Oktoba 28, 2020 unafanyika kwa njia ya amani.
Taarifa ya jana, Jumatatu, iliyotolewa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Gutteres, inasema mchakato shirikishi wa uchaguzi na ushiriki mpana wa vyama vya siasa na wagombea wao, haswa wanawake, unabaki muhimu kwa kulinda maendeleo yaliyofanywa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha utulivu, demokrasia na maendeleo endelevu.
Ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wafuasi wao kushiriki katika uchaguzi huo kwa amani na kujiepusha na visa vya vurugu.
Serikali pia imetakiwa kutoa mazingira salama ambayo yatawawezesha Watanzania kutekeleza haki yao hiyo ya kiraia na kisiasa.
