×

Matajiri Wavamia Kambi ya Yanga SC

BILIONEA na Rais wa Makampuni ya GSM, Ghalib Said Mohammed jana jioni aliongoza msafara wa matajiri wa timu hiyo kuvamia kambi ya Yanga waliyoweka kwenye Kijiji cha Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya kikao na wachezaji wao.

 

Hiyo ni katika kuelekea Dar es Salaam Dabi itakayopigwa leo saa 11:00 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar katika mchezo wao wa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu.

 

Katika mchezo huo, benchi la Yanga litaongozwa na Kocha Mkuu mpya Mrundi Cedric Kaze ambaye yeye itakuwa dabi yake ya kwanza tangu ajiunge na timu hiyo. Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, matajiri hao walivamia mazoezi hayo kwa ajili ya kuongeza hamasa na morali ya wachezaji pamoja na benchi la ufundi ili kuhakikisha wanawafunga watani wao wa jadi.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa viongozi walianzia kwa kutazama mazoezi ya mwisho ya timu hiyo yaliyofanyika jana saa kumi jioni kwenye Uwanja wa Avic Town ambako wamepiga kambi yao tangu kuanza kwa msimu huu.

 

Aliongeza kuwa matajiri hao baada ya mazoezi hayo, walikula chakula cha usiku pamoja sambamba na kufanya kikao cha pamoja na wachezaji hao na kutoa ahadi ya fedha kama wakipata ushindi, taarifa zinasema kuwa mabosi wameanza kwa kuahidi Sh 150Mil ambazo huenda zikaongezwa baadaye.

 

Matajiri wengine walioongozana na Ghalib ni mjumbe wa kudumu wa timu hiyo, Thobias Lingalangala sambamba na wale waliopo kwenye Kamati ya Mipango na Ushindi, Seif Magari, Abdallah Bin Kleb, Davis Mosha, Rogers Gumbo na Mjumbe wa Kamati ya Usajili ambaye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said.

 

“Matajiri wa Yanga wamedhamiria kufanya makubwa kwenye msimu huu na kitu cha kwanza ambacho wamepanga kukifanya ni kuhakikisha wanauchukua ubingwa wa ligi ambao watani wao Simba wameuchukua mara tatu mfululizo.

 

“Kingine ni kuwafunga Simba mara zote watakazokutana nao kwenye ligi na mashindano mengine ikiwemo Kombe la FA, lengo ni kurejesha heshima ya timu iliyopotea kwa misimu mitatu mfululizo.

 

“Hiyo ndiyo sababu ya matajiri hao kuungana kwa pamoja katika msimu huu na kuanzisha kamati hiyo mpya ya mipango na ushindi ambayo inawahusisha matajiri tupu, lengo ni kutoa hamasa ya timu ikiwemo kutoa posho kwa wachezaji,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Frederick Mwakalebela kuzungumzia hilo alisema: “Ni kawaida kwa viongozi kukutana na kuzungumza na wachezaji siku moja kabla ya mechi, hatukuanza katika mechi hii dhidi ya Simba.

 

“Kikubwa lengo letu ni kutengeneza hamasa ya wachezaji ili wajue viongozi tupo nyuma yao kwa kutimiza majukumu yao ya uwanjani ili tufanikishe malengo yetu ya ubingwa wa ligi katika msimu huu kwa kuhakikisha tunachukua pointi zote tatu kwa kila mchezo.”

Wilbert Molandi, Dar es salaam

Leave a Comment