
MSANII wa Komedi nchini, Emmanuel Mathias maarufu kama ‘Mc Pilipili’ amemtaja Mbunge wa Buchosa, Mhe. Eric Shigongo kuwa ndiye mtu alimefanya atimize ndoto zake alizokuwa na nazo za kuwa mshereheshaji ‘Mc’ kwenye shughuli mbalimbali.
Pilipili ameyasema hayo leo Alhamisi, Novemba 12, 2020 wakati anafanya mahojiano na kwenye kipindi cha Bongo 255 kinachoruka saa 7 mchana mpaka saa 10 jioni kupitia +255 Global Radio.

“Nilikuwa namsoma sana Eric Shigongo, na ‘Abby Cool’ Abdalah Mrisho ambaye kwa sasa ni Meneja Mkuu wa Global Publisher, kwenye gazeti la Uwazi walinifanya niache kazi niliokuwa naifanya na kuamua kuja Dar es Salaam kufukuzia ndoto ya maisha yangu. Shigongo amekuwa akiwashauri vijana na kuwapa hamasa ili kujikwamua katika maisha yao.
“Amekuwa mtu mkweli kwani haogopi kuanika kwamba alikomea darasa la saba lakini hakukata tamaa, alipambana mpaka kufika hapa alipofika leo, na sote tunaona, simulizi ya maisha yake ni hamasa tosha kwa vijana wenye kiu ya mafanikio na wenye uthubutu,” amesema MC Pilipili.
Aidha, Pilipili ambaye aliacha kazi ya ualimu na kuibukia kwenye sanaa, ameongeza kuwa umahiri wake kwenye kazi yake ya kusherehesha umefanya kuitwa Mc wa Taifa kutokana na kupata mialiko sehemu mbalimbali hapa nchini.