
UKICHEZA na mwanamke kwa sheria za sasa utaozea jela au kupigwa faini ya mamilioni ya fedha.
Kama unabisha sema: “suuu” uone.
Mwanasheria wa Jukwaa la Watoto (CDF), Amina Alliy alipozungumza na UWAZI hivi karibuni alisema:
“Kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2020 ambayo iliwasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza 2015 kwa hati ya dharura, imeorodhesha adhabu mbalimbali, ikiwamo faini ya Shilingi milioni 50 au kifungo cha miaka saba kwa mtu atakayebainika kusambaza picha za ngono mtandaoni.”
Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), imesema hivi karibuni kuwa wanawake ndiyo wanaongoza kudhalilishwa mitandaoni kutokana na kuwa na tabia za kupiga picha zenye utata na kuzituma mitandaoni pamoja na kutumia simu za wapenzi wao kupiga picha za utupu na hivyo kuwaonya wanaofanya hivyo kwani watakutana na mkono wa sheria.
Mwanasheria Amina wa CDF katika mahojiano yake na UWAZI alisema, baadhi ya makosa yaliyoanishwa katika sheria hiyo katika kifungu cha 13 na 14 ni kutuma taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono na za utupu, udanganyifu unaohusiana na kompyuta, makosa yanayohusiana na utambuzi, kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na kusambaza picha za utupu za watoto.
Sheria hiyo katika Kifungu cha 48 inaipa mahakama mamlaka ya kutaifisha mali iliyopatikana kutokana na kosa lililofanywa na mhusika.
Sheria hiyo pia itawataka wote watakaobainika kufanya makosa hayo kuwasilisha hati zao za kusafiria kwa mamlaka husika hadi hapo watakapolipa faini au watakapokuwa wamemaliza kutumikia vifungo.
Pia, kifungu hicho kinaeleza kuwa mtu atakayebainika kusambaza picha za ngono, uasherati na matusi, atatozwa faini isiyopungua Sh30 milioni au kwenda jela miaka 10, mtu atakayesambaza picha za utupu atalipa faini isiyopungua Sh20 milioni au kwenda jela miaka saba.
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi na Utekelezaji wa Sheria na Masharti ya Leseni wa TCRA, Dk. Philip Filikunjombe hivi karibuni alibainisha kuwa takwimu wanazopokea katika mamlaka hiyo nyingi zinawahusu wanawake kudhalilishwa mitandaoni.
“Wanaodhalilishwa mitandaoni, dada zetu wanaongoza kwa sababu wanapenda kupiga picha na ni wachangiaji wakubwa wa masuala binafsi mitandaoni.
“Changamoto ya usumbufu wa picha zao kuchapishwa na watu wengine mitandaoni inawakuta kwa sababu ya tabia ya kutuma picha mitandaoni,” alisisitiza Dk. Filikunjombe.
Aliendelea kutolea mfano kuwa waathirika wa matukio hayo wanapofika TCRA kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya waliofanya uhalifu huo, hubainika kuwa walihusika kuzichapisha wenyewe.
“Unakuta dada aliweka picha kwenye mtandao kupitia ukurasa wake na labda wakati huo alikuwa na mpenzi wake ambaye wameshaachana na pengine yeye anatakiwa azifute, lakini anakuwa hakumbuki nywila (password) ya kuingia kwenye ukurasa wake,” alisema.
Alisema suala hilo pia linachangiwa na ugawaji wa nywila kwa watu wa karibu au wapenzi wao na tabia ya kupiga picha za utupu au kuzipokea na kuzihifadhi kwenye simu.
Aliwataka Watanzania kuepuka kutuma picha za udhalilishaji mitandaoni kwa sababu ni kosa kisheria na ili kuepuka usumbufu kwa sababu teknolojia imekua na picha inavyotumwa ni rahisi watu kuichukua na kuihifadhi.
Uchunguzi uliofanywa na UWAZI umebaini kuwa picha nyingi za udhalilishaji mitandaoni zinawahusu zaidi wanawake huku wahusika wa kuziposti wakiwa ni wanaume.
Aidha, imebainika kuwa sababu kubwa inayowafanya wanawake kuwa waathirika wakubwa wa tatizo hilo linatoka kwao kwa kujiweka wazi kuhusu masuala yanayohusu ngono na mapenzi.
Uchunguzi umeonesha kuwa, kuna baadhi ya akaunti kwenye kurasa za facebook na instagram zimefunguliwa na baadhi ya wanawake kwa lengo la kujiuza kimwili ambako picha chafu hupostiwa jambo linalowapa nafasi wanaume kupata picha hizo na kuzisambaza.
“Watu wa kwanza kushiriki vita hii ni sisi wanawake, tuache kujidhalilisha wenyewe mitandaoni.
“Maana si kweli kwamba wanaume huwa wanatuvua mavazi na kutupiga picha ni sisi tuojivua kwa lengo la kutekeleza nia ovu, tukiacha kujidhalilisha sisi kama mwanamke kwa picha chafu tabia hii itakoma,” alisema Monica Rafael mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam alipofanya mahojiano na mwandishi wetu kuhusu tatizo la picha chafu za wanawake kuenezwa kwenye mitandao ya kijamii.
STORI: MWANDISHI WETU