×

Baba Amkata Sime Mwanaye, Kisa Ushirikina

MTOTO mwenye umri wa miaka tisa, mkazi wa Kitongoji cha Batini, wilayani Gairo, mkoani Morogoro, amenusurika kifo baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya shingoni na baba yake mzazi aliyefahamika kwa jina la Yakobo Taolo (38), huku chanzo kikidaiwa kuwa ni imani za kishirikina.

 

 

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, SACP Wilbroad Mutafungwa, amesema  tukio hilo limetokea Novemba 15 mwaka huu, majira ya 7:00 usiku ambapo baba wa mtoto huyo alivamia chumba alicholala binti yake huyo, anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Kibedya na kuanza kumshambulia kwa sime ambapo kwa sasa anapatiwa matibabu katika kituo cha afya Gairo.

 

 

Ameongeza kuwa mara baada ya baba huyo kutekeleza tendo hilo la kutaka kuua alitokomea pasipojulikana kabla ya jeshi la polisi kumkamata akiwa nyumbani kwa Robert Chidaka (45), mkazi wa Kibedya ambaye anashikiliwa na jeshi hilo.

 

 

Amefafanua kuwa baada ya baba huyo kushikiliwa na polisi, alianza kuumwa na kukimbizwa katika Kituo cha Afya Gairo kwa ajili ya matibabu na baadaye aligundulika kuwa na tatizo la kupumua na ilipofika alfajiri ya Novemba 16 mtuhumiwa huyo alipoteza maisha.

Leave a Comment