
SANJANA RISHI hivi karibuni aliamua kuvalia suti katika harusi yake badala ya mavazi ya kitamaduni ya bibi harusi wa Kihindi yenye muundo wa gauni la shela kwa sababu anapenda suti.
Lakini katokana na chaguo la vazi la siku ya harusi yake, pia aliwasilisha ujumbe mkubwa katika ulimwengu wa mitindo ambao umewaacha baadhi ya watu wakitafakari ikiwa wakati umewadia kwa mabibi harusi kuachana na kasumba ya kitamaduni na kuvalia suti.
Katika nchi za Magharibi, mtindo wa mabibi harusi kuvalia suti umepata umaarufu katika miaka ya hivi karibuni. Wanamitindo wamekuwa wakijumuisha suruali ndefu katika mavazi mkusanyiko wa nguo za harusi na zimeungwa mKono na wasanii maarufu.
Mwaka jana, muigizaji wa filamu ya ‘Game of Thrones’, Sophie Turner ,alivalia suruali ndefu nyeupe alipofunga ndoa na mwanamuziki Joe Jonas mjini Las Vegas. Lakini, mavazi ya Bi Rishi hayakuwa ya kawaida India- ambako bibi harusi huvalia sari (sketi ndefu, blauzi- na mtandio). Rangi inayopendelewa zaidi ni nyekundu iliyo na marembo ya dhahabu au fedha.

Bi Rishi, 29, mfanyabiashara wa India aliye na uraia wa Marekani, alioana na mfanyabiashara wa Delhi, Dhruv Mahajan, 33, tarehe 20 Septemba, 2020, katika mji wa Delhi. Aliwahi kufanya kazi ya uwakili nchini Marekani kabla ya kurejea India mwaka jana na wapenzi hao wamekuwa wakiishi pamoja kwa karibu mwaka mmoja sasa.
Walikuwa wamepanga kufanya harusi yao mwezi Septemba nchini Marekani ambako ndugu yake bibi harusi na baadhi ya marafiki wake wanaishi, na harusi ya pili ambayo ingelikuwa ya utamaduni wa kihindi ifanyike mjini Delhi mwezi Novemba.
Lakini mwishoni mwa mwaka janGa la Covid-19 lilipotokea mipango yao ”ikasambaratika kabisa”. Tofauti na Marekani, uhusiano wa wachumba kuishi pamoja kabla ya kuoana rasmi hairuhusiwi nchini India.
Bi Rishi anasema japo wazazi wake “walikuwa hawana tatizo na uamuzi wa mimi na mchumba wangu kuishi pamoja kabla ya kuoana, kulikuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa jamaa na marafiki kuwataka wafanye rasmi uhusiano wetu. Kwa hivyo mwisho wa mwezi Augosti, Asubuhi moja niliamka na kuamua, ‘acha tuoane’”.

Bi Rishi anasema alipoamua kuolewa alijua anataka muonekana wa aina gani na atavalia nini. “Nilijua nitavalia suti na nilijua ni suti aina gani,” alisema.
Alipokuwa akifanya kazi ya uwakili nchini Marekani, alipendelea sana kuvalia sana suti kwani “ndiye mwanamke wa kisasa niliyemhusudu. Nimekuwa nikivutiwa sana na mwenendo wa wanawake wanaovalia suti. Hali iliyonifanya kuvutiwa na vazi hilo na kulivalia muda lote.”
“Waliohudhuria walilikuwa wazazi wetu na babu na bibi zetu. Harusi ilifanyika nyumbani kwa kina Dhruv. Kila mmoja alikuwa amevalia mavazi ya kawaida tu, ningelikuwa tofauti sana laiti ningelivalia mavazi halisi ya harusi.”
Bwana Mahajan anasema hakutarajia mchumba wake atavalia suti.

Nguo ya harusi ya Bi Rishi ilisababisha gumzo mtandaoni. Baada ya kuweka picha ya mwonekano wake kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, marafiki walimpongeza sana ana kusifia nguo yake baadhi yao wakimpatia jina la “Bibi harusi wa kisasa”.
Wanamitindo wa mavazi pia walimpongeza kwa kuchagua vazi hilo la kipekee. Katika ujumbe walisema ameaibisha jamii na utamaduni wake, na kumuonya mama wake kuwa ameoana na mtu ambaye anatafuta sifa na ambaye yuko tayari kufanya lolote kwa jina la kupigania haki za wanawake.
Baadhi yao walisema hawezi kuelewa utamaduni wa Kihindi kwa sababu mawazo yake yametekwa na utamaduni wa magharibi.
“Wengine “waliniambia niende nikajiue,” anasema.

Bi Rishi anasema haelewi wanaomkosoa kwa sababu “Wanaume wa Kihindi huvalia suruali ndefu wakati wa harusi na hakuna anayewakosoa – lakini mwanamke anapofanya hivyo kila mmoja anamjadili”.
Siyo nchini India pekee ambako wanawake wanapigania haki ya kivaa suruali ndefu. Jitihada hizo zimekuwa zikiangaziwa kote duniani huku tamaduni nyingi hata katika jamii ya kisasa ikimhukumu mwanamke anayejaribu kuachana na vazi la nguo za jadi kwa wanawake.
Hadi mwaka 2013, ilikuwa vibaya kwa wanawake kuvaa suruali ndefu nchini Ufaransa japo marufuku hiyo imepuuziliwa mbali kwa miongo kadhaa. Nchini Korea Kusini, wanafunzi wa kike waliruhusiwa hivi karibuni kuunua suruali badala ya sketi ambayo ilikuwa sehemu ya sare zao.

Mwanafunzi wa kike huko North Carolina, Marekani, alilazimika kwenda kotini ili aruhusiwe kuvaa suruali shuleni wakati wa msimu wa baridi kali. Katika jimbo la Pennsylvania, msichana wa miaka 18 alikabiliana kisheria na shule yake kupata haki ya kuruhusiwa kuvaa suruali ndefu mwaka jana na kushinda.
Visa vya wanawake kuzuiwa kuvaa suruali vinaendelea kushuhudiwa nchini India. Japo Bi. Rishi anasema alipoamua kuvalia suti hakuwa anajaribu kuwasilisha ujumbe wa kisiasa, hata hivyo, ameafiki kuwa wakati mmoja ataingia ulingoni.