
KUNA barua iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuhusu staa wa Bongo Fleva, William Lymo ‘Billnass’ kuwa alipeleka barua ya posa kwa wazazi wa mchumba’ke, Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’. Taarifa ikufikie kwamba, mama mzazi wa Nandy, Maria Charles Mfinanga, amekataa katakata kujua chochote juu ya barua hiyo kisha akatoa la moyoni.
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA baada ya kusambaa kwa taarifa za posa hiyo, Mama Nandy alisema;
“Hiyo barua haina uhusiano wowote na familia ya Nandy na hatujaiona sisi kama familia.
“Hayo mambo hatuyajui na hatuelewi kinachoendelea kati yao, maana tunasikia tu mambo mengi, mara hivi, mara vile, lakini hatuelewi chochote.
“Hakuna kitu chochote kinaendelea kati ya hao watu wawili (Nandy na Billnass).
“Unajua kuna kitu watu hawakijui vizuri, Nandy amezaliwa kwenye familia inayojielewa mno na ndiyo maana tunashangaa mambo yanayoendelea huko kwenye mitandao.
“Bado suala la ndoa halijawa rasmi na hatujapokea chochote kwa maara ya posa kama watu wanavyosema.
“Siku jambo hilo la ndoa likiwa rasmi, tutasema, lakini kwa kweli kuhusu hiyo barua tunashangaa tu vitu vinavyoendelea kati ya wawili hao,” anasema Mama Nandy akisisitiza kwamba familia yao siyo watu wa kuongeaongea mambo mengi.
Kabla ya mama huyo kutoa la moyoni, mapema wiki iliyopita mitandaoni kulisambaa barua ambayo ilisemekana ilitoka kwa Billnass kwenda kwa wazazi wa Nandy ambapo ilipokelewa kwa mikono miwili hivyo kilichobaki ni ndoa tu.
Katika ujumbe ambao aliuposti kwenye ukurasa wake wa Instagram, Nandy alidokeza hilo kwa kifupi. “Nimepokea ujumbe, barua yake imepokelewa nyumbani… (wife to be…)”
Katika mazungumzo na mwandishi wetu mwingine, Nandy aliendelea kusisitiza kwamba, kwa sasa uchumba wake umekuwa rasmi baada ya barua hiyo.
Uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA WIKIENDA umebaini kwamba, Nandy na Billnass wamekuwa kwenye uchumba ambao una makengeza na kwamba kinachoonekana, wazazi wa mrembo huyo hawaliafiki jambo hilo.
Nandy alivishwa pete ya uchumba na rapa Billnass mapema mwaka huu. Kwa sasa wawili hao wanafanya vizuri na wimbo wao wa Do Me.
STORI: IMELDA MTEMA, DAR