
MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Benard Jordan maarufu Fundi Mitambo anayetamba ngoma mpya ya Sosomola ambaye hivi karibuni ziliibuka taarifa zake na muigizaji wa Bongo Muvi, Shamsa Ford kutoka kimapenzi mambo yamekuwa si shwari baada ya mke wa jamaa kutimba jijini Dar, kumsaka muigizaji huyo hali iliyoonekana kuanza kwa zengwe mapemaa.
Hivi karibuni mwanamuziki huyo alionekana kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii akimmwagia sifa za kimahaba hadharani muigizaji huyo na kutamka kuwa amempenda kutoka moyoni hali iliyopelekea amzawadie ngoma yake hiyo ya Sosomola.
Chanzo cheti cha habari kimedai kuwa ubuyu huo ulizagaa kwa kasi ya moto wa kifuu mpaka kuwafikia wapambe wa mke wa jamaa ambao inasemekana nao walimfikishia mkewe (jina halikuweza kupatikana mara moja) na kumjaza maneno hali iliyosababisha afunge safari kutoka Jijini Mwanza wanakoishi na kuja Dar kwa ajili kumsaka muigizaji huyo.
Chanzo hicho kimezidi kudai kuwa mwanamke huyo ameshaingia jiji la Dar na kuwatafuta wenyeji wake ili wamsaidie kumsaka muigizaji huyo anayetishia amani ya ndoa yake.

Kufuatia sakata hilo mwanahabari wetu alimtafuta Fundi Mitambo kwa njia ya simu na kumuuliza kuhusu sakata hilo ambapo alikiri mkewe kumfuata jijini Dar na kusema hiyo ilisababishwa na taarifa alizopewa na wapambe ambazo hakikuwa na ukweli wowote.
“Mimi ni mwanaume naweza kupenda wanawake idadi yeyote nnayoitaka hata kama nimpenda Shamsa sioni dhambi ila kuna wapambe ambao wamempelekea mke wangu taarifa kwa kuzitia chumvi na kuongeza ushabiki wao ndizo zilizomfanya atoke Mwanza tunakoishi kuja Dar.
“Hata hivyo nashukuru Mungu baada ya kufika nimemuelekeza nilipofikia akaja na kunikuta niko peke yangu nikakaa naye na kumuweka sawa ndipo roho yake ikatulia.

“Alinibana maswali mengi sana kuhusu uhusiano wangu na Shamsa ndipo nilimuelezea ukweli kuwa yule ni rafiki yangu na hatuna uhusiano wa kimapenzi na kumtaka asisikilize maneno ya wapambe.
Fundi alianza kujizolea umaarufu kwenye Bongo Fleva miaka kadhaa iliyopita alipotoka na ngoma ya Nakonda ndipo mwishoni mwa wiki iliyopita akaibuka Sosomola ngoma ilizua hekaheka hizo.
Mwanahabari wetu alipomtafuta Shamsa kuzungumzia sakata hilo alipokea simu na baada tu ya mwandishi kujitambulisha alimkatia simu na baada ya hapo haikupatikana tena.