
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amemsimamisha kazi Mkurugenzi Muendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Sabra Issa Machano na watendaji wengine kwa tuhuma za kuhusika na makosa mbali mbali katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya Serikali.
Dk. Mwinyi ametoa kauli ya kuwasimamisha watendaji hao wakati alipozungumza na Viongozi na watendaji wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) katika ukumbi wa taasisi hiyo uliopo Victoria Garden, Vuga Jijini hapa.
Watendaji wengine waliohusika na hatua hiyo ni pamoja na Ramadhani Abdalla Ali pamoja na watendaji wa Kamati nzima ya Uratibu wa mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) kutoka Wizara ya Fedha.
Alisema amechukua uamuzi wa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa ZSSF Sabra Issa Machano pamoja Ramadhani Abdalla Ali kwa makosa ya kiutendaji katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Jumba la Treni liliopo Darajani.
Alisema ni dhahiri kuwa katika utekelezaji wa mradi huo taratibu zilikiukwa na hivyo akabinisha ulazima wa kufanyika uchunguzi, wakati ambapo watendaji hao wakiwa nje ya kazi.
Alisema makosa dhidi yao hayatoi fursa ya wao kuendelea na kazi , hivyo ni vyema wakae pembeni kupisha uchunguzi na kusema Serikali itasimamia haki na kamwe hakuna mfanyakazi atakaeonewa dhidi ya tuhuma zinazowakabili.
Aidha, alisema hafurahishwi na utekelezaji wa mradi wa ZUSP uliogharimu Dola Milioni 93, ambao ulikusudiwa kuondoa changamoto mbali mbali katika Manispaa.
Alisema taarifa zilizopo zinaonyesha kuwepo makosa makubwa katika manunuzi pamoja na kufanyika udanganyifu juu ya kazi zilizoelezwa kufanyika, il-hali hazikufanyika.
Alisema amelazimika kuisimamisha Kamati nzima ya Uratibu wa Mradi huo ili uchunguzi uweze kufanyika, wakati wafanyakzi hao wakiwa nje ya kazi zao.

Vile vile Dk. Mwinyi aliagiza ZAECA kufanya Uchunguzi wa kina dhidi ya Mfanyakazi wa TRA Haidar Mussa Maisara anaetuhumiwa kushusha kiwango cha kodi katika tukio la kuingizwa Bandarini kichwa cha Scania, sambamba na Kampuni ya KEVIS aliyoaguiza ifanyiwe uchunguzi.
Alisema mfanyakazi huyo alijenga dhamira ya kujihusisha na rushwa, ambapo kwa nyakati tofauti aliteremsha kiwango cha kodi hiyo hadi kufikia shilingi Milioni tano, fedha ambazo haziendani na thamani halisi ya kodi iliyopaswa kulipwa, ambapo hatimae gari hilo lilitolewa usiku bila fedha hizo kulipwa.
Alisema anasikitishwa na miradi mikubwa jinsi ilivyogubikwa na matatizo makubwa kiasi ambacho haionyeshi thamani ya fedha zilizotumika na hivyo akaahidi kuchukua hatua mara moja dhid ay wote waliokiuka kanuni z amanunuzi.
Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi alisema tangu Serikali ya Awamu ya nane iingie madarakani imebaini kuwepo matatizo makubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa, na hivyo akasisitiza dhamira ya Serikali ya kuchukua hatua madhubuti.