
KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck amefunguka kuwa bado anaimani kubwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika katika mchezo wa pili wa michuano hiyo dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe kwa kuwa anaamini kikosi chake.
Simba imepoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kipigo cha bao 1-0 katika mchezo uliopigwa wiki hii kabla ya mchezo wa marudiano ambao utapigwa Januari 6, mwaka huu.

Akizungumza na Championi Jumamosi,Sven alisema bado wananafasi kubwa ya kufuzu hatua ya makundi licha kupoteza mchezo wa kwanza kwa kuwa watacheza kwenye uwanja wa nyumbani huku akiamini kwenye maandalizi yake.“
Nadhani bado nafasi ya kufuzu ipo ikiwa tutaendelea kufanya maandalizi ya nguvu kwa sababu hatukupoteza mchezo wa kwanza kutokana na ubora wapinzani bali imetokea kutokana na makosa ambayo tulifanya wenyewe.“
Unajua tunachokiangalia kwa sasa ni mchezo wa pili, tunacheza nyumbani, tutakuwa na nguvu kubwa ya kupambana, kikubwa kwa sasa ni kuangalia timu inataka nini kiufundi baada ya kuwaona wapinzani wetu, tunataka matokeo makubwa nyumbani,” alisema Sven
Stori: Ibrahim Mussa,Dar es Salaam