
RAIS John Magufuli amewataka Watanzania kuzitumia mvua zinazoendelea kunyesha kwa kulima mazao ya biashara ili kuziuzia nchi zinazokabiliwa na janga la Corona, huku akimtaka mkandarasi wa daraja la Kigongo, Busisi, kuimaliza kazi hiyo ndani ya miaka mitatu na si miaka minne.

Amesema hayo leo Jumatatu, Desemba 28, 2020 wakati alipofanya ziara ya kushitukiza katika daraja hilo linalotarajiwa kukamilika kwa gharama ya sh. bilioni 700.

“Watanzania tunatakiwa kumshukuru Mungu kwa kutuepusha na janga la Corona na tulime kwa nguvu zote ili kukuza uchumi wa nchi na watu kwa ujumla, kwani mazao mtakayolima tutaziuzia nchi zinazokabiliwa na Corona maana watu wao hawafanyi kazi wapo kwenye karantini,” amesema.

Amewaasa wananchi walime sana maana mwakani nchi inaweza kukabiliwa na janga la njaa kwa vile nchi nyingi zitahitaji chakula kutoka Tanzania.

Aidha, amemtaka mkandarasi anayejenga daraja la Kigogo Busisi wa Kampuni ya China Civil Engineering Group Limited kwa gharama ya Tsh. bilioni 700, kujenga mradi huo usiku na mchana ili kukamilisha ndani ya miaka mitatu, maana ilitakiwa iishie.kwa muda wa miaka minne.

Daraja hilo lililopewa jina la Magufuli lenye urefu wa kilomita 3.2 na barabara unganishi kilomita 1.66, ni la kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kwa kukuza uchumi wao.

Na Leah Marco, MWANZA