×

Watuhumiwa 683 Tabora Wakutwa na Silaha, Pembe za Ndovu, Sare za Jeshi

JESHI la Polisi limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 683 wa makosa mbalimbali mkoani Tabora katika oparesheni iliyochukua wiki tatu katika wilaya zote za mkoa huo.

 

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Opareshemi Maalumu za Jeshi la Polisi Tanzania, Kamishina Mwandamizi wa Jeshi wa Polisi (SACP) Mihayo Msikhela, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Tabora.

 

Alisema miongoni mwa watuhumiwa hao ni 277 wamefikishwa mahakamani na kuhukumiwa , watuhumiwa 255 bado kesi zao zinaendelea na watuhumiwa 42 wako katika uangalizi wa polisi baada ya kutokuwepo kwa ushahidi madhubuti.

 

SACP Msikhela alisema baadhi ya vielelezo vilivyokamatwa ni silaha aina ya gobore moja, mapanga tisa, meno ya tembo mawili, pikipiki 34 , magodoro 10 na simu za mkononi nne.

 

Vitu vingine vilivyokutwa kwa watuhimiwa ni vyuma vya reli viwili, runinga za aina mbalimbali 19, mfano wa sare za majeshi mbalimbali ya ndani na nje na pombe haramu ya gongo lita 408.

 

Aliongeza kuwa miongoni mwa watuhumiwa hao wamefanikiwa kukamata raia mmoja wa nje kabila yake Mhutu akiwa na aina mbalimbali za mfano wa sare za polisi na majeshi mengine.

 

Ameongeza kwamba mtuhumiwa huyo akikamatwa baada ya polisi kumwona amevaa sare ambazo zinafanana na za polisi lakini mshono wake ni tofauti.

 

Alisema baada ya kupekua begi alililokuwa amebeba  walikuta sare zinazotaka kufanana na zile za Jeshi la Wananchi na nyingine zinafana na za majeshi ya nje.

 

Katika operesheni hiyo ya kuanzia tarehe 7 mwezi huu, alisema, wamebaini kuwa magenge yanayojihusisha na uvunjaji wa nyumba, uporaji na wizi ni vijana ambao umri wao ni kuanzia miaka 15 hadi 21.

 

Alisisitiza kuwa  Jeshi la Polisi litaendelea kufanya oparesheni na misako ya mara kwa mara kwa kushirikiana na raia wema ili kukomesha uhalifu mkoani Tabora.

NA TIGANYA VINCENT

Leave a Comment