
MBUNGE wa Buchosa, Mhe. Eric Shigongo, na familia yake, leo Ijumaa, Januari Mosi, 2021, wamefanya ibada ya misa kuwaombea marehemu wazazi wake; Mzee James Bukumbi (baba yake mzazi) na Bi. Asteria Kapera (mama yake mzazi) ambao wameshatangulia mbele za haki.

Ibada hiyo imefanyika nyumbani kwao Shigongo katika Kijiji cha Bupandwamhela Halmashauri ya Buchosa.
Shigongo ametoa shukrani zake wa ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria ibada hiyo na kusema kuwa familia yake imeamua kufanya ibada ili kuwakumbuka wazazi wao pamoja na kuanza mwaka mpya kwa kumtengemea Mungu.

Shigongo ametumia nafasi hiyo kutoa ujumbe kwa wananchi wa Buchosa kuwapeleka watoto wao shule mara tu zitakapofunguliwa ili waweze kupata elimu ambapo amewaeleza kuwa kipaumbele chache kikubwa ni elimu kwa watoto, hivyo ni lazima wazazi wapeleke watoto wao shule na kuhakikisha wanasoma hata wakirudi majumbani.

Amesema anatarajia kuzindua kampeni yake ya “Buchosa Mpya, Peleka Mtoto Shule” ambapo atasaidia kutoa sare za shule, madaftari na vifaa vingine vya masomo kwa watoto wanaotoka familia duni na mayatima katika jimbo zima la Buchosa ili kusaidia watoto hao kusoma kwa raha na kufikia ndoto zao.




